Rais William Ruto anaonekana kuwa mwenye hasira na hofu akilaumu upinzani kwa kufeli kwa serikali yake. Na muda mfupi baada ya kumlaumu aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua, kwa kuongoza jaribio la mapinduzi na kushiriki vitendo vya kigaidi, Gachagua aliondoka nchini Jumatano usiku kwa ziara ndefu Amerika.
Hili linaonyesha jambo moja kubwa. Kumpindua rais kwa kutumia nguvu kinyume cha katiba ni uhaini – mojawapo ya makosa makubwa zaidi kwa mujibu wa sheria, ambalo linaweza kuadhibiwa kwa kifo. Ugaidi pia ni kosa zito, linalohusisha kifungo cha muda mrefu au hata adhabu ya kifo iwapo vifo vinatokea.
Katika hali ya kawaida, haiwezekani mtu anayetuhumiwa kwa uhaini, ugaidi na makosa mengine yanayogusa usalama wa taifa kuruhusiwa kuondoka nchini kwenda ziara ya nje. Polisi wangekuwa wa kwanza kumzuia hata kufika uwanja wa ndege. Mtu wa aina hiyo angekamatwa, na polisi wangeomba kibali cha mahakama kumshikilia kwa muda zaidi uchunguzi ukiendelea.
Kwamba Gachagua aliruhusiwa kuondoka siku hiyo hiyo ambayo Rais Ruto alitoa onyo kali kufuatia ghasia za Saba Saba, kuwa hakuna atakayesamehewa, ni ishara kubwa kuwa serikali haiko tayari kumkamata kiongozi yeyote wa upinzani.
Gachagua, ambaye sasa ameibuka kuwa kiongozi wa upinzani tangu kutengana na Rais na baadaye kuondolewa kupitia bunge, anaonekana kulengwa kwa lawama kutoka kwa serikali tangu maandamano ya Gen Z yaanze Juni mwaka jana. Serikali imekuwa ikielekeza lawama kwake na eneo lenye ushawishi la Mlima Kenya, kwa maandamano yaliyojaa ghasia yaliyochochewa na vijana, yaliyofikia kilele Juni 25 na Saba Saba.
Kiongozi huyo wa chama kipya cha Democracy for Citizens, sasa amekuwa sura na sauti ya juhudi za kuunda muungano wa upinzani.
Ziara yake ya miezi miwili Amerika, inayotajwa kuwa ya kukutana na Wakenya wanaoishi humo, inaonekana kama njia ya kujiondoa mstari wa mbele wa siasa na kuwaachia wengine kama Kalonzo Musyoka (Wiper), Martha Karua (People’s Liberation Party), Eugene Wamalwa (Democratic Action Party) na Fred Matiangi, ambaye bado hajajiunga rasmi na chama chochote, lakini anahusishwa na Jubilee cha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Iwapo vyombo vya usalama haviko tayari kumkamata Gachagua licha ya matamshi makali kutoka kwa Rais Ruto, Naibu wake Kithure Kindiki, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen, na maafisa wengine wa serikali na wabunge, ni wazi hawatamgusa hata kiongozi mwingine yeyote wa upinzani.
Kwa mujibu wa baadhi ya washirika wake wa karibu, ziara ya Gachagua si ya kukutana tu na Wakenya wa nje, bali ni mbinu ya kujiondoa kwenye lawama za moja kwa moja na kuipokonya serikali kisingizio cha kumlaumu kila wakati.
Haijulikani wazi viongozi wenzake wa upinzani watafanya nini wakati wa kutokuwepo kwake, lakini mikutano ya kitaifa itaendelea.
Huenda hali ikatulia kwa muda kama serikali haitafanya makosa ya kawaida ambayo huzua hasira kwa vijana. Baada ya kumshirikisha Raila Odinga serikalini kufuatia machafuko ya Juni mwaka jana — hasa kuvamiwa kwa Bunge na waandamanaji wa Gen Z — Rais Ruto alidhani hali imetulia. Lakini sasa amegundua kuwa ilikuwa ni afueni ya muda kabla ya dhoruba kuu.
Kifo cha mwanablogu Albert Ojwang akiwa rumande kilizua ghadhabu, zilizochangia vurugu kabla ya kumbukumbu ya Juni 25. Ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji, hasa kupigwa risasi kwa mchuuzi Boniface Kariuki, kiliongeza hasira.
Vifo 38 siku ya Saba Saba na 19 vya kumbukumbu ya maandamano ya Gen Z vimeonyesha sura ya serikali dhalimu inayowaruhusu polisi kutumia nguvu za kupindukia.
Kauli ya Waziri Murkomen iliyoeleweka kama amri ya ‘piga ua’ ilizua hasira. Hata 'marekebisho' ya Rais alipowaambia polisi wapige risasi miguu badala ya kuua, hayakusaidia.
Pia, licha ya ahadi ya Rais kusitisha vitendo hivyo, kikosi maalum cha DCI, kitego cha kukabiliana na ugaidi na NIS bado kinaendelea kuwateka washukiwa wa maandamano na kuwazuilia kinyume cha sheria au hata kuwaangamiza.
Kauli za Rais baada ya Saba Saba zinaonyesha hana nia ya kubadili msimamo licha ya lawama nyingi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu.
Lakini sasa anakabiliwa na hali ngumu ambapo makubaliano ya kumshirikisha Raila hayakuzima hasira za raia. Ngome za Raila zilikuwa kitovu cha maandamano ya awali, lakini sasa ni vijana kutoka maeneo tofauti nchini, hasa Mlima Kenya, wanaoibua changamoto kubwa zaidi.
Mpango wa kisiasa unaonekana ni kubebesha lawama Mlima Kenya. Wanasiasa wa UDA cha Ruto na ODM cha Raila wamekuwa wakilalamika kuwa eneo hilo, lililowahi kutoa marais watatu kati ya watano, linapinga serikali kwa sababu ‘mmoja wao’ hayuko madarakani.
Kuna juhudi za kufufua mpango wa “41 dhidi ya 1” wa mwaka 2007, ambapo Raila, Ruto na Mudavadi waliungana dhidi ya Kibaki.
Lakini safari hii mpango huo unaleta mwamko mpya Mlima Kenya, ambao awali haukuwa na ushawishi katika maandamano ya ghasia. Uharibifu, uchomaji mali, na mapambano ya wazi na polisi katika kaunti kama Nyeri, Kiambu, Nyandarua, Kirinyaga, Meru, Nakuru na zingine za Mlima Kenya umekuwa wa kiwango cha juu kuwahi kutokea.
Serikali imelaani vurugu, lakini kutoka kwa matamshi ya washirika wa kisiasa wa Ruto, ni wazi kuwa baadhi yao wanasherehekea hali hiyo kama ushahidi wa uasi unaoanzia Mlima Kenya.
Sasa wanapanga ziara za kisiasa kuhubiri madhara ya maandamano kwa uchumi na usalama wa mali.
Serikali pia inapanga kampeni ya amani itakayoongozwa na viongozi wa dini, wafanyabiashara maarufu, wanamuziki na watu mashuhuri kutoka Mlima Kenya.
Iwapo hili litafanikiwa ni suala la kusubiri kuona. Lakini kampeni ya #IamKikuyu na #WeAreAllKikuyus mitandaoni imekuwa jibu la moja kwa moja kwa matusi ya kisiasa, huku watu kutoka maeneo mengine wakijitambulisha na jamii hiyo.
Vitisho vya Rais kukabiliana na wanaodaiwa kuwa na njama ya kuipindua serikali vimepata uungwaji mkono kutoka kwa ngome zake, lakini kuna pia sauti za wastani zinazomhimiza kusikiliza kilio cha wananchi.
Pendekezo la Raila Odinga la kikao cha kitaifa linaweza kufungua mwanya wa suluhisho. Raila, bingwa wa siasa za maandamano tangu miaka ya 1990, sasa anaonekana kutaka mjadala badala ya maandamano.
Hii inaashiria kufufua BBI ya 2018 au makubaliano ya 2022 yaliyolenga kutuliza hali baada ya uchaguzi.
Hata hivyo, mapendekezo hayo hayatatui masuala makubwa yaliyozua maandamano ya Gen Z: ukosefu wa ajira, ukabila, ufisadi, gharama ya maisha, ukiukaji wa haki, pengo kati ya maskini na matajiri, na maisha ya anasa ya viongozi.
Mashirika ya kijamii na baadhi ya wapinzani tayari wamekataa pendekezo la Raila wakilitaja kuwa njia ya kujitafutia nafasi ya mamlaka.
Lakini ukweli unabaki kuwa, bila mazungumzo ya kweli na wazi, mambo hayawezi kutatuliwa. Bila hivyo, uchaguzi wa 2027 utakuwa wa kugombanisha taifa lililogawanyika vibaya.
from Taifa Leo https://ift.tt/WuPUpAL
via IFTTT