Katwa Kigen asema hatampendelea Ruto kesi ya uchaguzi 2027 akiingia Mahakama ya Juu

MASUALA ya uadilifu na kutopendelea upande wowote yalitawala wakati Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) ilipohoji walioorodheshwa kwa nafasi ya jaji wa Mahakama ya Juu, huku wanaomezea mate wadhifa huo wakidadisiwa kuhusu mali, mienendo yao ya awali na uhusiano wa kisiasa.

Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Katwa Kigen, alikabiliwa na maswali makali kuhusu uhusiano wake na Rais William Ruto alipokuwa wakili wake na athari zake iwapo kutakuwa na kesi ya uchaguzi wa urais mwaka 2027, huku aliyekuwa mwenyekiti wa IPOA, Anne Waceke Makori, akikosolewa kwa kushindwa kuwasilisha maelezo ya mali inavyotakiwa.

Mwaniaji wa tatu, Jaji wa Mahakama Kuu Joseph Sergon, alikabiliwa na malalamishi kuhusu alivyoshughulikia kesi nyeti ya kisiasa inayohusisha chama cha Wiper Patriotic Front.

Mijadala hiyo ilionyesha wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa makamishna wa tume, chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu Martha Koome, kuhusu iwapo wagombea wanaweza kuaminika na umma kuhudumu katika mahakama hiyo ya juu zaidi, hasa kuelekea uwezekano wa mzozo wa uchaguzi wa urais mwaka 2027.

Suala la uwezekano wa kesi ya uchaguzi wa urais mwaka 2027 liliibuka mapema katika mahojiano hayo, na kuongoza sehemu kubwa ya maswali.

Makamishna walimkabili Jaji Kigen kuhusu hofu kwamba kazi yake ya zamani ya kuwakilisha Rais Ruto inaweza kudhoofisha imani ya umma katika uhuru wake iwapo atahusika katika kesi ya uchaguzi.

Hata hivyo, Jaji Kigen alikiri kuwa aliwahi kumwakilisha Dkt Ruto, ikiwemo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), lakini akasisitiza hilo halitaathiri maamuzi yake.



from Taifa Leo https://ift.tt/fHKa0Fn
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post