
MIAKA miwili baada ya maandamano makubwa ya vijana wa Gen Z yaliyotikisa nchi na kulazimisha serikali kuondoa Mswada wa Fedha wa 2024, athari zake bado zinaonekana wazi kusumbua serikali hasa katika sera za ushuru, uchumi na siasa za kitaifa.
Miaka miwili baadaye, Gen Z wameonyesha kuwa sauti ya vijana inaweza kubadilisha sera za serikali na kuathiri maamuzi makubwa ya kitaifa.
Hata hivyo, kwa maelfu ya Wakenya wanaoendelea kukabiliwa na gharama ya juu ya maisha na kwa waliobeba makovu ya maandamano hayo, mapambano yao bado hayajaisha.
Jana, kulikuwa na wasiwasi serikalini huku vijana hao wakipanga maadhimisho ya maandamano hayo.
Polisi walisema hawataruhusu umati kukusanyika popote jijini sawa na ilivyokuwa mwaka jana ambapo watu kadhaa walikufa.
Kauli ya Mkuu wa polisi wa Nairobi Issa Mahammud ilijii baada ya mikutano kadhaa ya maafisa wakuu wa usalama na kauli zao kwamba, hawatakubali uhuni kutatiza shughuli jijini na maeneo mengine nchini.
Mnamo Jumanne, Rais Ruto alihutubia taifa kufafanua Sheria ya Fedha 2026 aliyotia saini akisema haijaanzisha ushuru mpya. Hii ilionekana kama hatua ya kutuliza vijana hao wanapoadhimisha maandamano hayo leo.
Maandamano hayo yaliyoanza kama upinzani dhidi ya ushuru mpya 2024 yaligeuka shinikizo kubwa kudai uwajibikaji serikalini na kupinga gharama ya juu ya maisha.
Sasa wachambuzi wanaamini kuwa Gen Z walizua mwelekeo mpya ambao umefanya serikali kuwa makini zaidi inapopanga sera za ushuru.
Kabla ya maandamano hayo kuzuka Juni 2024, Rais William Ruto alikuwa ameweka wazi azma yake ya kuongeza kiwango cha ushuru kinachokusanywa na serikali kutoka asilimia 14 ya pato la taifa hadi asilimia 16 ifikapo mwisho wa mwaka huo na kufikia kati ya asilimia 20 na 22 kabla ya kumaliza muhula wake.
Akizungumza katika Ikulu Mei 2024, Rais alisema ongezeko la ushuru lingesaidia serikali kupata fedha zaidi za maendeleo na kupunguza kutegemea mikopo.
Hata hivyo, maandamano yaliyoongozwa na vijana kupitia mitandao ya kijamii yalivuruga mipango hiyo.
Zaidi ya watu 60 walifariki kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu huku mamia wakijeruhiwa na mali ya thamani ya mabilioni ya shilingi kuharibiwa.
Kutokana na upinzani huo, Mswada wa Fedha wa 2024 uliondolewa na serikali kulazimika kubadilisha mkakati wake wa ukusanyaji ushuru.
Takwimu za Wizara ya Fedha zinaonyesha kuwa, kiwango cha ushuru kama sehemu ya pato la taifa kilishuka kutoka asilimia 13.8 mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 13.3 mwaka wa 2024/25 baada ya kufeli kwa mswada huo.
Serikali sasa imeepuka kuanzisha ushuru mpya mkubwa na badala yake imeelekeza nguvu katika kuboresha ukusanyaji mapato na kuhakikisha watu wengi zaidi, hasa katika sekta isiyo rasmi, wanalipa ushuru.
Mabadiliko hayo yanaonyesha jinsi maandamano ya Gen Z yalivyolazimisha serikali kubadili mkondo wake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo ya kisiasa, changamoto ya gharama ya maisha ambayo ilichochea maandamano hayo bado haijaondoka.
Uchambuzi wa bei za bidhaa muhimu unaonyesha kuwa kikapu cha bidhaa saba za kawaida za chakula kiligharimu Sh1,101 mnamo Mei mwaka huu ikilinganishwa na Sh1,068 mwezi Juni 2024 wakati maandamano yalipoanza.
Bei ya unga wa mahindi wa kilo mbili imeongezeka kutoka Sh134 hadi zaidi ya Sh159 huku mafuta ya kupikia yakipanda kwa asilimia tisa.
Bei ya sukuma wiki nayo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 32 katika kipindi hicho.
Kwa familia nyingi za kipato cha chini, ongezeko hilo lina maana ya kutumia sehemu kubwa zaidi ya mapato yao kununua chakula kuliko ilivyokuwa miaka miwili iliyopita.
Mfumuko wa bei ya vyakula pia umeongezeka kutoka asilimia 5.6 mnamo 2024 hadi asilimia 9.4 Mei mwaka huu, jambo linaloonyesha kuwa gharama ya maisha ingali juu.
Wakati huo huo, baadhi ya vijana walioshiriki maandamano hayo bado wanaishi na majeraha ya kimwili na kisaikolojia.
Minnie Gathoni ni mmoja wao.
Alipigwa risasi mkononi akiwa karibu na nyumbani kwake Waithaka wakati wa maandamano ya Juni 25, 2024.
Risasi tatu ziliharibu mifupa na mishipa ya mkono wake wa kushoto. Madaktari walifanya upasuaji mara kadhaa kuokoa mkono huo, lakini hadi leo hawezi kuutumia kikamilifu.
“Mkono wangu si kama ulivyokuwa awali. Siwezi kubeba vitu vizito wala kufanya kazi nyingi za nyumbani,” anasema.
Mbali na maumivu ya mwili, anasema ameathirika kisaikolojia na mara nyingi hulia anapokumbuka yaliyompata.
Kijana mwingine, Eugene Arogo mwenye umri wa miaka 24, bado uhisi maumivu ya kifua baada ya kujeruhiwa na mkebe wa gesi ya kutoa machozi uliomgonga usoni wakati wa maandamano karibu na Bunge.
Anasema hadi sasa, hana uwezo wa kununua dawa kila mara kutokana na ukosefu wa ajira.
“Wakati mwingine nalazimika kuvumilia maumivu kwa sababu sina pesa za dawa,” anasema.
Licha ya majeraha yao, vijana hao wanasema wataungana tena na wengine kuadhimisha kumbukumbu ya maandamano ya Gen Z leo na kuwakumbuka waliopoteza maisha.
Kwa wengi wao, maandamano hayo hayakuwa tu kuhusu ushuru bali pia kuhusu haki, uwajibikaji na nafasi ya vijana katika kuamua mustakabali wa nchi.
from Taifa Leo https://ift.tt/lKEsGyU
via IFTTT