Wanaume wengi wahepa ndoa wakidai ni mzigo

IDADI ya wanaume wanaochelewesha au kukwepa kabisa kuoa katika miaka yao ya 30 na 40 inaongezeka, huku wengi wakisema ndoa imekuwa mzigo wa kifedha, kihisia na hata kisheria.
Hayo ni kwa mujibu wa mkufunzi wa masuala ya mahusiano na maisha, Jeff Israel Nthiwa, ambaye anasema wanaume wengi wanafika katika kituo chake cha Destiny Life Coaching wakieleza kwa nini hawaoni sababu ya kuingia kwenye ndoa kwa sasa.
“Kwa wanaume wengi, ndoa ni sawa na maumivu. Hesabu wanazofanya ni za kifedha, kihisia na hata kisheria. Wanauliza ikiwa ndoa itarahisisha maisha yao au kuyafanya kuwa magumu zaidi,” alisema.
Kwa mujibu wake, wanaume wengi hutazama ndoa zinazowazunguka lakini hawazioni kama mifano ya upendo wa kudumu. Anasema wengi huingia kwenye ndoa wakitarajia kupokea mapenzi lakini baadaye huhisi jukumu lao ni kutoa pekee.
“Mwanaume hapaswi kuoa akitarajia kupendwa. Ndoa si biashara ya kubadilishana mapenzi. Ukifikia kiwango cha kutoa mapenzi bila kutarajia malipo, ndipo unakuwa tayari kwa ndoa,” alisema.
Jeff anaamini mzigo unaowekwa kwa wanaume katika ndoa ni mkubwa kwani wanatarajiwa kuwa wachumaji wa riziki, viongozi na wabebaji wa majukumu ya kifedha na kihisia, huku watu wachache wakijiuliza wao wenyewe wanahitaji nini kutoka kwa wenzi wao.
Kuhusu wanaume wanaogeuza miadi ya kwanza kuwa kama mahojiano ya kazi, Jeff alisema tabia hiyo si nzuri kwa sababu mahusiano yanapaswa kuanza kwa kujenga uelewano.
“Tunapaswa kuanza kwa kufahamiana. Nataka kuelewa mahitaji yako na wewe uelewe yangu,” alisema.
Katika ushauri anaowapa wanaotarajia kufunga ndoa, Jeff huwashauri wachunguze kwanza ikiwa kila mmoja ana uwezo wa kutimiza mahitaji ya mwenzake.
“Shughulikieni msingi kabla haujavunjika. Wengi wetu tunashughulikia nyufa za ndoa badala ya msingi wake,” alisema.
Aidha, alipinga dhana kwamba wanaume huchelewesha ndoa kwa sababu hawana pesa.
 “Tatizo si fedha, bali ni mtazamo. Mwanaume wa kweli huanza na maono. Mwanamke anayefaa ni yule anayeelewa maono hayo na kuyasaidia,” alisema.
Jeff alieleza kuwa mapenzi hupitia hatua mbalimbali. Hatua ya kwanza ni pale mtu anapompenda mwenzake kwa sababu anataka kupata kitu kutoka kwake. Hatua ya pili ni pale mtu anapojipenda vya kutosha kiasi kwamba anaweza kutoa mapenzi bila kutegemea malipo.
Hatua ya tatu, ambayo alisema watu wachache huifikia, ni ya kutoa mapenzi bila masharti yoyote.
Alitoa onyo kwa wanaume na wanawake wanaoingia kwenye mahusiano kwa kutegemea pakubwa hisia.
“Jikamilishe kwanza kabla ya kutafuta mtu wa kukupenda,” alisema.
Pia, aliwataka wanaume wasikimbilie ndoa bila kujenga msingi wa urafiki na uchumba. “Wanaume wengi huona uchumba kama kupoteza muda. Lakini usikimbilie ndoa. Baada ya miaka 10 ya kesi mahakamani ndipo utagundua ungechukua muda kumjua mwenzi wako,” alisema.
Kwa mujibu wake, mahusiano ya siri yasiyo na uwajibikaji ndiyo huwafanya wengi kuumia zaidi.Akizungumzia wanaume waliokulia katika familia zenye migogoro ya ndoa, Jeff alisema historia ya wazazi haipaswi kuamua maisha ya watoto wao. “Uzoefu wa mtu mwingine si lazima uwe uzoefu wako. Wengi wetu tumetoka katika familia zilizovunjika. Ndio maana ni muhimu kila mmoja ajiponye kwanza kabla ya kuingia kwenye ndoa,” alisema.
Aliongeza kuwa lawama kati ya wanaume na wanawake ndizo zinazochangia kuvunjika kwa mahusiano.
Kuhusu dhana kwamba wanaume wana muda mwingi wa kusubiri kabla ya kuoa kwa sababu thamani yao huongezeka wanapozeeka, Jeff alisema hilo pia lina gharama zake.
“Utapoteza maono yako. Jiulize una muda gani wa kulea familia. Hesabu nyingi ambazo wanaume wanafanya kuhusu kusubiri si sahihi,” alisema.


from Taifa Leo https://ift.tt/cuH671d
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post