Maseneta waambia Mbadi, Lee na Wahome wapunguze kiburi wafike mbele yao

MAWAZIRI watatu sasa wanaandamwa na maseneta kwa kiburi kutokana na kukosa kuitikia mialiko ya kuhudhuria vikao vya mabunge ya seneti. Wao ni Waziri wa Fedha John Mbadi, mwenzake wa Ardhi Alice Wahome na Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui. Mawaziri hao wamekashifiwa mno huku Bw Mbadi akiwa pabaya maseneta wakitishia kuitisha kikao cha kujadili mienendo na madharau yake. Bw Mbadi mapema mwezi huu alikataa kufika seneti akisema alikuwa ameshughulishwa na majukumu mengi. Wiki jana aliambia seneti kuwa hangefika dakika 30 kabla ya kuanza kwa kikao ambacho alikuwa akitarajiwa kujibu maswali kuhusu wizara yake. Bw Mbadi pia alikataa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Fedha na Bajeti kwenye Seneti akihiari kuhudhuria mkutano wa kisiasa katika Kaunti ya Migori kisha kufika kwa mahojiano na kituo kimoja cha runinga baadaye jioni. Miezi miwili iliyopita, Maseneta walimwonya Bw Mbadi akome kudharua seneti na kuichukulia kama baraza la kijiji ambako anaamua mwenyewe iwapo atafika au la. Aidha, wiki jana alikataa kufika mbele ya Kamati ya Fedha na Bajeti ya Seneti kuzungumzia makadirio ya bajeti na mikakati iliyowekwa kupunguza deni la taifa bila kuwaumiza raia kupitia ushuru mwingi. Aliwataka maseneta watumie wasilisho ambalo alilitoa alipofika mbele ya Kamati ya Fedha na Bajeti kwenye Bunge la Kitaifa kujibu hoja walizokuwa wameibua. Bi Wahome naye yupo matatani kwa kukosa kufika mbele ya seneti mara saba. Wiki jana hakufika kujibu swali la Seneta wa Mombasa Mohamed Faki ambaye alitaka kufahamu masuala yanayohusu ardhi, uchafuzi wa mazingira na kuhamishwa kwa maskwota. Bw Faki na Seneta wa Kiringa James Murangó walisema Bi Wahome alikuwa ameonyesha wazi anadharau seneti na kukosa kufika kujibu maswali ya kimsingi. Bi Wahome hata hivyo aliwaomba maseneta wamruhusu afike mbele yao kati ya Mei 12 na Mei 15. Bw Kinyanjui pia amekosa kufika mbele ya maseneta mara mbili lakini akajitetea kuwa bado alikuwa mgeni kwenye wizara hiyo na alikuwa akilainisha mambo ili kufahamu mengi yaliyokuwa yakiendelea. Alikuwa amekosa kufika mbele ya kamati ya biashara inayoongozwa na Seneta wa Kwale Issa Juma. Maseneta waliowakashifu mawaziri hao hasa walimlenga sana Bw Mbadi ambaye walisema amewaonyesha madharau ya wazi. Spika Amason Kingi amewataka maseneta watumie mamlaka yao kuwaadhibu mawaziri ambao hawafiki mbele yao.

from Taifa Leo https://ift.tt/aVQkzuG
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post