
MKUTANO wenye hisia kali wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) uliofanyika Jumanne uliamua kuunda timu ya kitaalamu ili kupitia upya mkataba uliopo kati ya kiongozi wa chama Raila Odinga na Rais William Ruto. Mkutano huo ulioongozwa na Bw Odinga ulitangaza mipango ya kushirikiana na timu kutoka chama cha Rais Ruto, United Democratic Alliance (UDA), kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa ajenda 10 kwenye Mkataba wa Makubaliano (MoU) uliotiwa saini mwezi Machi. Kamati Kuu ya Usimamizi iliyokutana jijini Nairobi pia iliunga mkono uamuzi wa Bw Odinga wa kushirikiana na Rais Ruto chini ya mpango wa Serikali Jumuishi, angalau hadi mwaka 2027. Tangazo hili lililenga kumaliza mkanganyiko kuhusu msimamo wa chama katika kushirikiana na Rais Ruto, hasa baada ya Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, kutangaza kuwa mkataba huo umekufa kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelea, ikiwemo utekaji nyara na mauaji yanayotekelezwa na polisi chini ya utawala wa Kenya Kwanza. Katika mkutano wa faragha uliodumu kwa saa kadhaa,
Taifa Leo imebaini kuwa ulikuwa na mchakato mzuri lakini wenye hisia kali, huku baadhi ya maafisa wakimuonya Sifuna kwa maoni yake. Bw Sifuna amekuwa mkosoaji mkali wa serikali ya Dkt Ruto, akisema haitekelezi makubaliano kati ya ODM na UDA. Huku baadhi ya wenzake wakiahidi kumuunga mkono Ruto kwa muhula wa pili, Bw Sifuna amekuwa wazi kusema Rais hana sifa za kuongoza tena. Hata hivyo, Sifuna aliungwa na baadhi ya maafisa, huku mkutano ukishinikiza kukosolewa kwa utawala wa Rais Ruto kwa ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelea. Pia mkutano ulieleza wasiwasi kuhusu matumizi makubwa ya mali na fedha za serikali na baadhi ya maafisa wakuu wakati taifa linakumbwa na uhaba wa pesa. Katika makubaliano yao ya Machi, Rais Ruto na Bw Odinga walikubaliana kulinda na kuimarisha ugatuzi, kuheshimu haki ya kukusanyika na maandamano ya amani, kulipa fidia waathiriwa wa maandamano na kuheshimu sheria na katiba. Hata hivyo, serikali ya Kenya Kwanza imeendelea kuwakamata bila sababu wakosoaji. “Kulikuwa na hisia kuwa Katibu Mkuu amekuwa akisababisha mkanganyiko; baadhi ya wajumbe walisema kama kila afisa atatoa maoni yake binafsi kuhusu mambo ya chama, basi kutakuwa na machafuko,” alisema afisa mmoja aliyehudhuria mkutano. “Hata hivyo, wajumbe walieleza wasiwasi kuhusu ukiukaji unaoendelea wa haki za binadamu; suala la kukamatwa na utekaji wa watu wanaoshutumiwa kuwa wakosoaji wa serikali. Lakini pia walihisi kuwa licha ya baadhi ya ajenda kutotekelezwa kikamilifu, kuna maendeleo fulani. Walihisi pia kuwa wawakilishi wa chama walioteuliwa kuwa mawaziri wanahitaji msaada wa kutosha ili wafanye kazi yao,” alisema afisa mwingine. Mkutano uliagiza Kiongozi wa Wachache Bungeni, Junet Mohammed, na mwenyekiti wa ODM, Gladys Wanga, kuongoza kuundwa kwa timu ya kitaalamu. Maafisa walibainisha kuwa timu hiyo itajumuisha watu wasio wanasiasa. Chama pia kilitangaza kuunga mkono Bw Odinga kushirikiana na Rais Ruto kuleta utulivu na kuanzisha mazingira bora kwa Wakenya kushughulikia masuala yao kwa njia za kidemokrasia na kikatiba. Mkutano uliibua wasiwasi kuhusu utekelezaji kamili wa mapendekezo ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa, ikilenga kulinda haki ya kukutana kwa amani, utawala wa sheria, katiba, kupambana na ufisadi na matumizi mabaya ya rasilmali za umma. Mnamo Mei, Bw Odinga alitetea kauli ya Sifuna akisema yeye ndiye msemaji rasmi wa chama. “Mwishowe, msimamo rasmi lazima uelezwe na chama, na msemaji rasmi wa chama ni Katibu Mkuu, Sifuna. Yeye husema kwa niaba ya chama,” alisema Bw Odinga. Katibu Mkuu amekuwa akikosoa vikali ukiukaji wa haki za binadamu, ukatili wa polisi, utekaji nyara na mauaji ya kiholela. Ameweka wazi kuwa ODM si sehemu ya serikali na haitamsaidia Rais Ruto katika uchaguzi wake wa muhula wa pili.
from Taifa Leo https://ift.tt/iN1mh2a
via
IFTTT