Wabunge wapinga mpango wa kuweka mbolea katika orodha ya bidhaa zinazotozwa ushuru wa VAT

WABUNGE wamepinga mpango wa kuweka mbolea katika orodha ya bidhaa zinazotozwa ushuru wa VAT kama ilivyo katika Mswada wa Fedha wa 2025 wakisema utaathiri vibaya wakulima, na kufanya gharama ya uzalishaji wa chakula kupanda.

Mswada huo, ambao kwa sasa upo mbele ya Kamati ya Fedha na Mipango ya Bunge la Kitaifa unalenga kuifanya mbolea kuwa katika orodha ya bidhaa zisizotozwa ushuru wa VAT.

Hata hivyo, katika kikao na Kamati ya Bunge ya Bajeti (BAC), Mbunge wa Molo Kuria Kimani, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya fedha, alisema kwamba anafanya kila awezalo kuhakikisha kwamba mbolea inasalia katika orodha ya bidhaa zisizotozwa ushuru wa VAT.

 “Pendekezo hili ni jambo linalohitaji kupelekwa polepole kwa sababu kuhamisha mbolea hadi inayotozwa ushuru wa VAT, kutaongeza bei yake na hatimaye kufanya gharama ya maisha kuwa juu," alisema Bw Kimani.

Mbolea inayotumika humu nchini inatengenezwa humu humu, kumaanisha kuwa kuiweka katika mfumo usio wa moja kwa moja wa kutoza ushuru kutaathiri mchakato wa utengenezaji wa bidhaa za humu nchini ambazo zimeajiri mamia ya Wakenya.

Ingawa Mswada huo haupendekezi ushuru wowote wa ziada kwa mbolea, kufanya mageuzi hayo kuna athari mbaya kwa walengwa.

Hii ina maana kwamba wakulima watalazimika kununua bidhaa hiyo kwa bei ya juu jambo ambalo litaathiri pakubwa uzalishaji wa chakula nchini.

Haya yanajiri huku Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino akionya kwamba isipokuwa uainishaji upya uliopendekezwa hautabadilishwa, gharama ya chakula nchini itapanda maradufu na hivyo kuwaathiri Wakenya ambao tayari wanakabiliwa na gharama ya juu ya maisha.

"Ikiwa serikali itapandisha gharama ya mbolea jinsi Mswada huu unavyopendekeza, gharama ya chakula itapanda na hivyo basi kuua sekta ya kilimo ambayo inachangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi" alionya Bw Owino.

"Tunahitaji kuhimiza utengenezaji wa bidhaa za ndani ili kuwezesha serikali kubuni nafasi za kazi. Lakini hili haliwezi kutokea ikiwa tutawaathiri wakulima kupitia bei ya mbolea. Mambo lazima yabadilike kwa maslahi ya Wakenya," Mbunge wa Embakasi Mashariki aliongeza huku Mbunge wa Molo akitoa hakikisho kwamba "kila kitu kiko sawa."

Mbunge huyo wa Molo pia alibaini kuwa kamati yake imepanga kukutana na watengenezaji wa mbolea wa humu nchini ili kujadili suala hilo.

Kenya ilianzisha VAT kwa mara ya kwanza mnamo Januari 1, 1990 na bidhaa nyingi ambazo zilitumika katika sekta ya kilimo kama vile mbolea na mbegu zilikadiriwa kuwa zimeondolewa kwenye VAT.

Baadhi ya biashara za kilimo-kwa mfano, zinazouza mayai na maziwa -- hazingehitimu kusajiliwa kwa vile zilikuwa zikizalisha na kusambaza bidhaa ambazo hazijaruhusiwa.



from Taifa Leo https://ift.tt/5dVIERG
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post