JIONI ya Juni 22 2024, baada ya siku ndefu ya kuratibu mawakili kote nchini waliokuwa wakitafuta vijana waliotekwa nyara na kupotea, Rais wa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK), Faith Odhiambo, alikuwa akijaribu kupumzika nyumbani kwake. Lakini muda si muda, simu ya dharura ya LSK ilipigwa. Sauti iliyokuwa upande wa pili ilisema kwa haraka: “Billy the Goat ameachiliwa na yuko eneo la Muthaiga.” Huyo ni mtumiaji maarufu wa mitandao aliyekuwa amepotea. Bila kusita, Bi Odhiambo, ambaye ilikuwa miezi minne tu tangu achaguliwe, aliwajulisha baadhi ya mawakili wenzake na akaanza safari kuelekea eneo hilo. “Tulimpata Billy akiwa katika hali mbaya. Alikuwa na njaa. Tulianza kwa kumnunulia chakula,” anasema. Wakiwa Galito’s wakimnunulia chakula, waliandaa video fupi iliyosambaa haraka mitandaoni. Kwa miezi sita iliyofuata, Bi Odhiambo alizuru vituo vya polisi kote Nairobi akiwaokoa vijana waliotekwa au kukamatwa kiholela, huku familia zao zikimtazama kama mkombozi dhidi ya ukandamizaji wa serikali. Alipochukua hatamu za uongozi wa LSK, aliahidi kurudisha chama hicho katika sifa zake kihistoria: kusimamia haki si kwa wanasheria tu, bali kwa Wakenya wote. Lakini hakutarajia kuwa atajikuta akiwa mstari wa mbele katika maandamano ya kizazi cha Gen Z dhidi ya Mswada tata wa Fedha, 2024 yaliyoishia kwa vifo, utekaji, na ukatili kutoka kwa vikosi vya usalama. Bi Odhiambo hakusita. Akiwa pamoja na baraza lake na mashirika ya kijamii, alikabiliana ana kwa ana na maafisa wa serikali na polisi. Alionekana kila siku kwenye nyumba vya mahakama na milango ya vituo vya polisi, akitafuta haki kwa waliodhulumiwa. Katika mahojiano ofisini kwake, katika kampuni ya wanasheria ya Ombok na Owuor LLP, anasema utulivu wa sasa unaweza kuwa tu kimya kabla ya dhoruba. Ana wasiwasi na hali ya ukandamizaji wa kisiasa, ukatili wa polisi, na kutoheshimu sheria. Maandamano ya Gen Z yalimuonyesha kuwa Wakenya wana utu – madaktari, wanahabari, wanasaikolojia, na wananchi walijitokeza kusaidia. Wahudumu wa mikahawa walitoa chakula na maji, huku LSK ikiongoza juhudi za kisheria. Alitoka nje ya ofisi na kwenda kushuhudia maafa wakati wa maandamano, akatupiwa vitoa machozi kwa mara ya kwanza alipokuwa akiwakomboa waandamanaji katika kituo cha polisi cha Central, Nairobi. Baadaye, polisi walikataa kuwaonyesha mahabusu waliokuwa wamekamatwa, lakini waliendelea kusimama kidete. “Walikuwa wakiwaleta usiku baada ya sisi kuondoka. Hii ilikuwa kinyume cha sheria,” asema. Wengi waliotekwa walipoachiliwa, walinyamaza, ishara ya mshtuko waliopitia. Ingawa polisi wanakana kuhusika, Bi Odhiambo anaamini ni kazi ya maafisa wa serikali. “Kila tunapotoa taarifa hadharani, vijana huachiliwa,” asema. Je, aliwahi kuhofia maisha yake? Alilengwa, lakini hakuwa akijali sana usalama wake binafsi, hadi alipogundua watu wenye silaha waliokuwa wakimfuata. Tangu hapo, alianza kuchukua tahadhari. Mumewe humsaidia sana, hata kumpeleka usiku katika vituo vya polisi. “Ameona mateso kwa macho yake. Na anaelewa kuwa hata dakika moja inaweza kuleta tofauti kubwa,” asema akimshukuru. Hatetei Wakenya tu. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania alimpigia kuhusu kutekwa kwa mwanaharakati Sarungi Tsehai. Bi Tsehai aliachiliwa kufuatia hatua za haraka za Bi Odhiambo na mashirika mengine. Wengi serikalini humuona kama msumbufu. Alipokataa uteuzi wa Rais Ruto kujiunga na kamati ya kukagua madeni ya taifa, baadhi ya wenzake walimkosoa. Lakini anasema, baraza lake lilikuwa nyuma yake kikamilifu. “Hatuwezi kuwa na utekaji nyara chini ya Katiba ya 2010 inayotoa haki madhubuti,” asema kwa msisitizo. Anaongeza kuwa upinzani kujiunga na serikali kumeondoa uangalizi wa kweli. LSK inasalia kuwa mstari wa mbele: ikiwasilisha kesi dhidi ya serikali kuhusu masuala kama Mkataba wa Adani, ushuru wa nyumba, kutumwa kwa wanajeshi mitaani, na kutengea matangazo ya serikali kwa KBC pekee. Kuhusu Mahakama, anasema: “Ikiwa wananchi hawaiamini Mahakama, wataingia barabarani. Gen Z waliandamana kwa sababu hawakuamini mahakama wala serikali kufuata maagizo yake.” Anaonya kuwa ghasia wakati wa uchaguzi zinaweza kurudi kama mahakama haitarejesha imani ya wananchi. Licha ya changamoto, ameanzisha mabadiliko makubwa ndani ya LSK: kuboresha wanachama, kukabiliana na matapeli wanaodai kuwa mawakili, na mpango wa kulea mawakili wachanga. Kwa wanawake, ujumbe wake ni: Ota ndoto kubwa. “Nilipojiunga na baraza, sikuwahi kufikiria ningekuwa rais. Wapo waliokuwa na mvuto zaidi. Lakini tazama nilipo sasa.” Kuhusu baadaye? “Kama ni siasa, siwezi sema kwa sasa. Lakini niko tayari kuhudumia Wakenya katika nafasi yoyote Mungu atakayofungua,” anasema kwa matumaini.
from Taifa Leo https://ift.tt/WXf7e9S
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS