MBABANE, ESWATINI
SERIKALI ya Eswatini imejitetea kuhusu hatua yake ya kuruhusu Amerika kuwatupa wahalifu sugu nchini humo, ikisema hatimaye itawarejesha wafungwa hao kwao.
Hii ni baada ya ndege kutoka Amerika kuwasafirisha wahalifu watano sugu hadi Eswatini ambako wamewekwa kwenye kifungo gerezani jijini Mbabane.
Hii ni kutokana na makubaliano ambayo ufalme wa Eswatini umeingia na utawala wa Rais Donald Trump wa kuruhusu Amerika kuwasafirisha wafungwa na wahamiaji haramu nchini humo.
Mnamo Jumanne ndege iliyowabeba wahalifu watano sugu ilitua Eswatini baada ya Mahakama ya Amerika kuondoa marufuku iliyoweka dhidi ya kuwazuia wahamiaji wasirejeshwe hadi mataifa yasiyo asili yao.
Wahalifu hao watano walikuwa wakitoka Vietnam, Jamaica, Laos, Cuba na Yemen. Amerika ilisema kuwa nchi zao zilikuwa zimekataa kuwapokea ndiposa wakapelekwa magereza ya Eswatini.
“Serikali inatambua hisia kali za raia kutokana na hatua ya kuwapokea wafungwa wa uhalifu kutoka Amerika hadi ufalme wa Eswatini,
“Ni ukweli wahalifu watano walisafirishwa nchini na wanazuiliwa kwenye magereza yetu kutokana na muafaka kati yetu na Amerika,” akasema Msemaji wa serikali ya Eswatini Thabile Mdluli.
Eswatini ni nchi ambayo haipakani na bahari Afrika Kusini na ina raia milioni 1.2. Taifa hilo limekuwa chini ya uongozi wa ufalme ambao umekuwa madarakani tangu 1986.
Ushirikiano na Amerika utashuhudia nchi hiyo ikiwapokea wafungwa sugu kisha kuwazuilia kabla ya kuwarejesha nchi zao za asili.
Hata hivyo, haieleweki jinsi Eswatini itafanya hivyo ikizingatiwa mataifa hayo yamekataa kupokea wafungwa hao kutoka Amerika moja kwa moja.
from Taifa Leo https://ift.tt/O7Ju6z1
via IFTTT