Kwa miaka mingi, eneo la Mlima Kenya limekuwa likishirikiana na Bonde la Ufa katika chaguzi tatu zilizopita za urais, na kuwasaidia kuingia madarakani Rais wa sasa William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.
Lakini inaonekana vijana wa Gen Z watabadilisha hali katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Ushindi wa Bw Kenyatta mwaka 2013 na 2017 katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti na uchaguzi wa marudio mwezi Oktoba pamoja na kuingia kwa Dkt Ruto madarakani mwaka 2022 kulichangiwa pakubwa na muungano wa maeneo hayo mawili.
Mipango kama hiyo ambapo miungano ya kisiasa huundwa kwa kuwakusanya viongozi mashuhuri kutoka makabila mbalimbali kwa ahadi ya kugawana nyadhifa serikalini, pia ilishuhudiwa katika chaguzi za awali za urais, ikiwemo mwaka 2002 wakati Mwai Kibaki alishinda kwa kushirikiana na wanasiasa mashuhuri waliowaleta pamoja wapiga kura wa maeneo yao.
Hata hivyo, hesabu hizi za kisiasa za jadi zinakabiliwa na changamoto kubwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku kizazi cha Gen Z, ambacho awali kilijiepusha na siasa, kikianza kushiriki kikamilifu.
Kizazi hiki kilichozaliwa kati ya mwaka 1996 na 2012, kinaibuka si tu kama kundi la wapiga kura, bali pia kama vuguvugu kali la kisiasa. Wamekataa kujitambulisha na wanasiasa wakuu wa jadi waliokuwa wakigawa nchi kwa misingi ya kikabila.
Uchambuzi wa sensa ya 2019 uliofanywa na Shirika la Takwimu la Kitaifa Kenya (KNBS) unaonyesha kuwa wengi wa Gen Z watakuwa wamefikisha umri wa kupiga kura kufikia mwaka 2027.
Wanne kati ya kila Gen Z watano, yaani zaidi ya watu 14 milioni, watakuwa wapiga kura, ongezeko la asilimia 79.4 kutoka mwaka 2022 ambapo Dkt Ruto alichaguliwa kwa kampeni aliyoahidi kuinua maisha ya vijana.
Wakenya wenye umri wa miaka 18 hadi 34 watakuwa 17.8 milioni, na watatoa mchango mkubwa katika kuamua mwelekeo wa kisiasa wa nchi kuanzia 2027.
Katika uchaguzi wa 2022, Dkt Ruto alipata kura 7,176,141 dhidi ya Bw Odinga aliyepata 6,942,930. Kulikuwa na wapiga kura waliosajiliwa 22.1 milioni lakini waliopiga kura walikuwa 14. 3 milioni pekee, kumaanisha watu milioni 8 hawakushiriki.
Ripoti ya IEBC ilionyesha kuwa idadi ya vijana walioshiriki uchaguzi mwaka 2022 ilikuwa ndogo sana. Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa wapiga kura 8,811,691 wenye umri wa miaka 18 hadi 34 walikuwa wamesajiliwa, sawa na asilimia 40 ya jumla ya wapiga kura kabla ya uchaguzi wa 2022. Idadi hiyo pekee ingeweza kubadili matokeo ya uchaguzi.
“Funzo lililo dhahiri ni kwamba Gen Z watakuwa na ushawishi wa kihistoria katika uchaguzi wa 2027 na uchaguzi utakaofuata,” anasema Bw Javas Bigambo, mchambuzi wa siasa.
Anasema vijana wanapaswa kuungana kwa misingi ya maadili na fikra wanapofanya maamuzi ili nguvu yao zizae matunda.
“Uwezo wa nguvu na ushawishi wao hauwezi tena kupuuzwa, na sasa wanatambua kuwa hawahitaji kuchochewa na mwanasiasa yeyote. Sasa wanapaswa kujifunza ustadi wa kudhibiti na kupata mamlaka ya kisiasa, lakini muhimu zaidi, waungane kwa misingi ya fikra, si hasira na ukosefu wa mwelekeo,” anasema Bw Bigambo.
Ikiwa Gen Z wataamua kuungana kwa misingi ya fikra na kuachana na siasa za kuabudu watu au kufuata wanasiasa wa maeneo yao kwa upofu, basi kuna uwezekano mkubwa wa kubadilisha kabisa hali ya kisiasa ya nchi.
Uchambuzi wa mienendo ya upigaji kura ya awali umeonyesha jinsi baadhi ya maeneo yamekuwa yakipigia kura kulingana na mwelekeo wa “viongozi wao wakuu”.
Mwaka 2022, wakati maeneo ya Mlima Kenya na Bonde la Ufa yalimunga mkono Dkt Ruto, yalileta pamoja karibu kura zote.
Kaunti 10 za Mlima Kenya na saba kutoka Bonde la Ufa zilimpa Dkt Ruto kura 4.5 milioni sawa na asilimia 63 ya kura zake zote, kulingana na data ya IEBC ya uchaguzi wa 2022.
Kaunti za Laikipia, Tharaka Nithi, Murang’a, Kiambu, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua, Embu, Meru na Nakuru zilimpa Rais Ruto karibu kura milioni tatu. Akiwa na kura 2,938,309 kutoka kaunti 10 za Mlima Kenya, Dkt Ruto aliongeza kura 1.6 milioni kutoka kaunti saba za Bonde la Ufa..
“Gen Z wanaweza kuondoa ushawishi wa viongozi wa kikanda. Hawawatambui viongozi hao. Hili linaweza kuleta mabadiliko makubwa mwaka 2027,” anasema Prof Macharia Munene, mhadhiri na mchambuzi wa siasa.
Hata hivyo, aliongeza kuwa baadhi ya viongozi bado wanaweza kuwa na ushawishi fulani.
Prof David Monda, mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika, anataja vijana kama nguvu kubwa ya mabadiliko ya kijamii—lakini anaonya kuwa ukabila bado utakuwa na nafasi katika siasa za 2027.
“Lakini tofauti ni kuwa haitakuwa sababu pekee au ya kipekee katika maamuzi ya wapiga kura. Masuala ya kiuchumi, utawala bora, haki kwa waliouawa kiholela na uwazi pia yatakuwa muhimu sana,” anasema Prof Monda.
“Kilicho muhimu hapa ni kuwa wimbi la Gen Z linaweza kuamua kura yenye ushindani mkali. Lakini ukabila bado ni kiini cha siasa za Kenya,” anaongeza.
Seneta wa Kitui Enoch Wambua anataja nguvu ya idadi ya Gen Z kama silaha kali inayoweza kubadilisha uongozi na utawala wa nchi.
“Hiki ni kizazi kilichounganishwa na mateso waliyopitia mikononi mwa viongozi wasiojali. Wanataka uwajibikaji mkubwa zaidi kutoka kwa viongozi,” anasema Bw Wambua.
from Taifa Leo https://ift.tt/SGNRKDg
via IFTTT