Wandani wa Ruto: Tuna kadi fiche ya ‘Tutam’

WANDANI wa Rais William Ruto wamesisitiza kuwa wana kadi kali fiche na mbinu nyingi ambazo watatumia kuangusha upinzani huku wakiweka wazi kuwa sasa wanavamia Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Licha ya dhana kuwa utawala wa sasa umewachosha raia kutokana na ahadi zisizotimizwa na kukiuka haki za kibinadamu dhidi ya waandamanaji, wandani wa Rais wameweka macho makavu kuwa lazima atahudumu mihula miwili. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, Waziri wa Afya Adan Duale na Kiongozi wa The Service Party Mwangi Kiunjuri wote wamesisitiza kuwa rais hatikiswi na watashinda kura inayokuja kwa mwanya mkubwa kiasi kwamba upinzani hautakuwa na njia zozote za kulalamika. Katika eneo la Mlima Kenya, viongozi hawa wameweka wazi watakuwa wakitumia mbinu ya tenga utawale kugawanya kura za eneo hilo ambalo kwa sasa linadhibitiwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. “Iwapo upinzani wanafikiria kuwa uwepo wetu ndani ya serikali umetumaliza kisiasa basi wamenoa. Siku inakuja ambapo tutayakunja mashati yetu na tuzamie siasa kali wala hawataamini rais akishinda kura ya 2027 kwa mwanya mkubwa,” akasema Profesa Kindiki akiwa Pwani mnamo Julai 5. “Kwa sasa tunamakinikia ujenzi wa barabara, kuunganisha maboma kwa umeme na kuhakikisha Wakenya wengi wanayapata maji na pia kuwapiga jeki wakulima. Haya ni mambo ambayo wapinzani wetu hawawezi kufanya na ndiyo tutayatumia kuwaangusha,” akaongeza. Kwa mujibu wa Bw Kiunjuri hawajaacha nyuma mpango wa kumvizia viongozi wa upinzani hasa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka. Viongozi hawa wanatumai kutakuwa na mpasuko kuhusu mwaniaji wa urais upinzani kisha watumie hilo kuwavutia wale watakaohisi wamedhulumiwa. “Nani alisema Rais Ruto anaondoka? Kutoka 2027 hadi 2032 kutakuwa na sura mpya lakini bado atakuwa rais,” akasema Bw Kiunjuri. “Rais alituambia tupuuze upinzani na nafahamu hilo kwa sababu mimi ni kati ya vinara ndani ya Kenya Kwanza,” akaongeza. Japo nguvu zimeelekezwa kwa Bw Musyoka, kuna pia uwezekano aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangí na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya pia wanatarushiwa chambo na serikali. Pia Rais Ruto yuko makini kufufua uhusiano wake ambao unaonekana kusambaratika na mtangulizi wake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta. “Siasa ni maslahi na hakuna uadui wa milele. Hawa wote unaowaona kwenye upinzani wakipewa dili bora, watakuja. Yule ambaye hatumtaki wala hatuwezi kushirikiana naye ni Gachagua,” akasema Bw Kiunjuri. Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi naye anasema kuna mpango fiche ambao wakiutoa tu, upinzani utalemazwa kabisa na hawatakuwa na mbinu zozote za kumkabili Rais Ruto. “Angalieni jinsi mambo yanavyoenda, huu upinzani utaporomoka kama mnara wa babeli,” akasema Bw Sudi. Naye Mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek alisema wanalenga kutumia sheria vilevile kupambana na viongozi wa upinzani. “Tunathmini kutumia kila sheria si kuwahukumu bali kuhakikisha uwajibikaji kwa wanaoendeleza chuki na uchochezi,” akasema Bw Kiborek. Rais Ruto mwenyewe amekuwa akikariri kuwa hana wasiwasi na upinzani utakuwa mswaki kwake debeni 2027. Kwa kipindi kimoja alisema kuwa hatatoa mamlaka kwa viongozi wa upinzani aliowarejelea kama watu wasiokuwa na maono. Baadhi ya wandani wake kama aliyekuwa Waziri wa Biashara Moses Kuria na Seneta Samson Cherarkey hata wamependekeza kuwa hakutakuwa na uchaguzi 2027 na hata muhula wa Rais Ruto unaweza kuongezwa. Bw Ichung’wah naye amekuwa akimrejelea Bw Gachagua kama kiongozi anayetumia machungu yake ya kibinafsi kuchochea nchi dhidi ya serikali ila wana mipango mahususi ya kummaliza kisiasa. Bw Gachagua alitimuliwa mnamo Oktoba 2024 baada ya kuhudumu kama naibu rais kwa miaka miwili. Kiongozi wa PLP Martha Karua ni kati ya wakosoaji wakubwa wa Rais Ruto na  amekuwa akisisitiza kuwa utawala huu umevuka mpaka kutokana na utendakazi  duni na dhuluma dhidi ya raia, kwa hivyo hauna njia zozote za kuwahi uongozi tena mnamo 2027. Gavana wa Murangá Irungu Kangáta na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ndio viongozi wa hivi punde wa Mlima Kenya kumwasi Rais Ruto huku wakilalamika kuwa vijana kutoka eneo hilo wamekuwa wakiuawa wakati wa maandamano.

from Taifa Leo https://ift.tt/5cFzsN3
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post