
NAIBU Inspekta Jenerali wa Polisi (DIG) aliyejiondoa kwa muda Eliud Lagat, anatarajiwa kurejea afisini Jumatatu, Julai 14, 2025 baada ya kuondolewa lawama kuhusiana na mauaji ya mwanablogu Albert Ojwang’. Jumapili jioni, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alithibitishia
Taifa Leo kwamba atarejea afisini kwa sababu chunguzi mbalimbali zimebaini kuwa hakuhusishwa na mauaji hayo. “Nataraji kumwona afisini kesho (leo) kwa sababu ameondolewa lawama na chunguzi zote,” Bw Kanja akathibitisha. Juhudi zetu za kumfikia Bw Lagat kupata kauli yake hazikufaulu kwa sababu hakujibu simu na jumbe fupi tulizomtumia. Naibu huyo wa Inspekta Jenerali wa Polisi alijiondoa afisini kwa muda mnamo Juni 16 ili kutoa nafasi kwa Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuendesha uchunguzi kubaini ikiwa alihusika na mauaji ya Ojwang’ ambaye pia alikuwa mwalimu. Hii ni kutokana na sababu kwamba Bw Lagat ndiye aliwasilisha malalamishi kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwamba Ojwang’a aliweka mitandaoni taarifa ya kumhusisha na sakata ya ufisadi. Hapo ndipo maafisa wa DCI kutoka Nairobi wakishirikiana na wenzao wa Homa Bay waliekea nyumbani kwa marehemu, eneo bunge la Kabondo Kasipul, na kumkata mnamo Juni 7, 2025. Walimsafirisha hadi Nairobi na akazuiliwa katika seli moja katika Kituo cha Polisi cha Central, ambako alidaiwa kupigwa na kuuawa mnamo Juni 8, 2025. Afisa mmoja wa IPOA mwenye ufahamu wa matokeo hayo aliambia
Taifa Leo kwamba uchunguzi wao haupata ushahidi unaohusisha moja kwa moja, Bw Lagat na mauaji ya Ojwang’. Mamlaka hiyo ilidida kusema lolote hadharani kuhusu uchunguzi ikitaja kesi zinazoendelea mahakamani ambapo Afisa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Central Samson Talaam na maafisa wengine wa kituo hicho ni miongoni mwa wale walioshtakiwa kwa mauaji hayo. Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Igonga alikuwa ameahidi kutoa kauli yake kuhusu suala hilo, lakini hadi tulipoenda mitamboni, Jumapili jioni, hakuwa amefanya hivyo. Wakati ambapo Ojwang’ aliuawa, iliaminika kuwa Bw Lagat ndiye aliwaagiza maafisa katika kituo hicho kumchapa na kumtesa mwanablogu huo. Baada ya kulemewa na presha, DIG huyo mnamo Juni 16 alitoa taarifa kutangaza kujiondoa kwake kwa muda. “Kwa moyo safi na kwa kuzingatia wajibu na majukumu yangu kama Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi na kwa misingi ya chunguzi zinazoendelea kuhusu kifo cha kusikitisha cha Albert Ojwang, nimeamua kujiondoa afisini mwa muda hadi chunguzi hizo zitakapokamilishwa. Naahidi kutoa usaidizi wowote, nikihitajika kufanya hivyo, wakazi wa uchunguzi kuhusu kisa hicho cha kusikitisha,” akaongeza Bw Lagat.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA
from Taifa Leo https://ift.tt/cJGiEM8
via
IFTTT