NDOA nyingi zinavunjika siku hizi si kwa sababu ya ukosefu wa mapato au usaliti wa kimapenzi, bali maneno yanayozungumzwa na wanandoa hasa katika nyakati za hasira.
Wataalamu wa masuala ya familia na washauri nasaha, wanasema kuwa maneno ya matusi, dharau, dhihaka na vitisho huacha majeraha ya kihisia ambayo hujenga ukuta wa uhasama na kufifisha mawasiliano ya kweli.
“Ndoa hujengwa juu ya misingi minne: upendo, heshima, uaminifu na mawasiliano. Lakini maneno hasi yanapozidi kutamkwa ndani ya ndoa, hata yale ya mzaha au ya hasira, hugeuka sumu inayoua misingi hiyo mmoja baada ya mwingine,” asema Farida Kalau, mshauri wa masuala ya ndoa.
Anasema moja ya kauli hatari zinazojitokeza mara kwa mara wanandoa wakigombana ni 'acha upuuzi' au 'acha ujinga'. Ingawa baadhi hujitetea wakisema inaonyesha kukerwa, kauli hizi humfanya mwenzi kujihisi duni au mjinga.
Vilevile, kauli kama 'unawezaje kuwa mjinga hivi?' au 'mwanaume wa aina gani wewe? Ni kama mimi ndiye mume hapa' huathiri sana heshima ya mume ndani ya ndoa.
Mwanaume anapopoteza nafasi yake ya kihisia kama kichwa cha familia, huwa mgumu kubadilika au kujihusisha tena kwa moyo wote katika majukumu ya ndoa.
Kwa upande mwingine kuna wanaume wanaofokea wake wao - 'mama yako hakukufundisha kuwa mke?' kauli inayowavunjia heshima wanawake. Unapodhalilisha mwanamke na familia yake, huwa unaondoa kabisa hali ya kukuamini.
Kauli hii ni kama mkuki kwa moyo wa mwanamke.Wapo pia wanaotumia maneno kama silaha: 'nimeshaamua na maamuzi yangu ni ya mwisho!' Kauli hii hufunga kabisa milango ya mazungumzo, majadiliano na maridhiano.
Katika ndoa, ushirikiano ni lazima. Mtu mmoja hawezi kuendesha ndoa kwa maamuzi ya upande mmoja kama dikteta.Katika hali ya hasira, baadhi ya wanandoa hutoa kauli kali kama 'ondoka kwenye nyumba yangu!' au 'nataka talaka!'
Hata kama kauli hizi hutamkwa kwa lengo la kumfanya mwenzi atafakari au abadilishe tabia, ukweli ni kuwa zinavunja msingi wa usalama wa kihisia.
Mwanandoa anapoambiwa na mwenzake “ondoka”, hujenga hofu ya kukataliwa, na 'nataka talaka' hugeuka kuwa tishio linalotumiwa kama njia ya kudhibiti mtu hali inayoashiria unyanyasaji wa kihisia.
“Kauli nyingine hatari ni 'wewe ni kahaba' ambayo huenda ikatamkwa kwa msingi wa tuhuma au wivu. Bila uthibitisho, kutumia matusi kama haya hakuleti suluhu bali huzua maumivu na uharibifu wa utu wa mwenzi wako.
Hii si tu ni dhihaka bali pia ni unyanyasaji wa moja kwa moja,” asema Kalau.Aidha, kauli kama 'sikupaswa kukuoa' au 'rafiki zangu walikuwa sahihi kukukataa' huathiri sana nafsi ya mwenzi wako.
Hujenga hali ya majuto na hisia za kutothaminiwa, hasa kwa mke au mume ambaye amewekeza hisia, muda na maisha yake katika uhusiano huo.
Wataalamu wa ushauri wa ndoa wanasema kwamba kabla ya kusema chochote, jiulize: “Je, maneno yangu yatajenga au yatabomoa?” Ikiwa yataleta hasara zaidi ya faida, ni heri kunyamaza, kutulia na kuzungumza baada ya hasira kupungua.
“Njia bora ya kushughulikia migogoro ni kuwasiliana kwa upole, kueleza hisia bila lawama, na kusikilizana kwa makini. Ndoa nyingi zimevunjika si kwa sababu ya tatizo kubwa, bali kwa sababu ya maneno yaliyotamkwa kwa hasira bila kutafakari,” asema.
Anasema katika dunia yenye changamoto za kila siku, ndoa zinahitaji ulinzi wa makusudi. “Wanandoa wanapaswa kuwa walinzi wa mioyo ya wenzao – si maadui wa kihisia ndani ya nyumba moja. Maneno ni silaha. Yakitumika vibaya, hujeruhi. Yakitumika vyema, huponya,” aeleza.
from Taifa Leo https://ift.tt/uhKnAMy
via IFTTT