WAZAZI wameelezea wasiwasi kwamba ukosefu wa shughuli za likizo na maeneo salama ya michezo huwaweka watoto katika hatari ya kuingizwa kwenye dawa za kulevya, dhuluma za kingono, ajira na hata uhalifu.
Huku shule zikipangiwa kufunga kwa likizo ya muhula wa pili wiki hii, wazazi wanasema huwa wanahofia kila wakati watoto wanapokaa nyumbani bila shughuli muhimu za kufanya.
“Mimi huondoka nyumbani saa kumi na mbili asubuhi kuuza mboga katika soko la Kongowea. Watoto wangu watatu hubaki nyumbani peke yao au kuenda kucheza mitaani. Kila siku huwa nina hofu. Lolote linaweza kutokea,” asema Bi Esther Atieno, mzazi katika Kaunti ya Mombasa.
Afisa wa afya ya jamii katika eneo la Tiwi, Kaunti ya Kwale, Bi Mebakari Ali, asema imebainishwa visa vingi vya unyanyasaji wa watoto, mimba za mapema, ajira kwa watoto, matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu unaowashirikisha watoto hutokea wakati wa likizo.
Haya yalithibitishwa na Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kwale, Bi Lilian Lewa, ambaye anasema visa vya unyanyasaji wa watoto huongezeka wakati wa likizo na kuwashauri wazazi kuwafuatilia watoto wao kwa karibu.
Bi Ali anasema watoto hasa kutoka vijijini na mitaa duni hujitafutia ajira katika machimbo ya kokoto na michanga, sehemu za kutengenezea pombe haramu, mashambani au kandokando ya bahari kuu ambako huweza kunyanyaswa kingono au kimwili.
Alionya kuwa matumizi ya mtandao bila mwongozo huweza kuwaweka watoto hatarini kuwindwa na wahalifu wa mitandaoni.
“Shule ndio mazingira ya pekee yenye mpangilio wanaoyajua watoto wengi. Likizo ikianza na watoto wako nyumbani kwa zaidi ya mwezi bila mtu wa kuwaangalia, wanakuwa rahisi kuingia kwenye mitego ya uhalifu au manyanyaso. Wazazi wengi hufanya kazi za vibarua na hawawezi kubaki nyumbani au kugharamia vituo vya kulea watoto. Tunahimiza jamii na viongozi wa mitaa wachukue hatua za mapema kuwasaidia watoto wakati wa likizo,” akaongeza.
Afisa wa watoto katika Kaunti ya Mombasa, Bw Gabriel Kitile, alipendekeza kuwa, wazazi waandae shughuli ambazo watoto wanaweza kufanya kila siku ili kuwaepushia madhara mitaani.
Baadhi ya taasisi za kidini na mashirika ya kijamii zimeingilia kati na kuweka mipango ambayo itahakikisha watoto wako salama wakati wa likizo.
Katika eneo la Kisauni, madrassa Swalihina imeandaa kambi ya wiki mbili ya mafundisho ya Quran na malezi kwa watoto wa kiume na wa kike walio kati ya miaka 9–14.
“Tunawafundisha kuhusu maadili, uwajibikaji na mbinu rahisi za maisha. Hii huwasaidia kuepuka mitaa hatari,” asema Sheikh Suleiman Walid, mratibu wa mpango huo.
Bi Abigael Ndizi, mratibu wa jamii na mshirikishi wa masuala ya afya ya uzazi kwa vijana kutoka shirika la Samba Sports Youth Agenda, alisema wanatekeleza mipango inayolenga kuwezesha jamii kuelewa kuhusu ukatili wa kijinsia (GBV), hasa kwa vijana wa kike na wa kiume.
from Taifa Leo https://ift.tt/wytfr7U
via IFTTT