
WAZIRI wa Kawi Opiyo Wandayi amesema kuwa katu hatabanduka kwenye kambi ya Rais William Ruto huku akikashifu upinzani kwa kupanga maasi dhidi ya serikali. Bw Wandayi amewataka Wakenya waheshimu Rais Ruto jinsi marais waliotangulia walivyoheshimiwa na wamruhusu achape kazi ili atimize ahadi alizotoa wakati wa kampeni. “Hoja kwamba mmechagua rais haimfanyi mateka wenu. Kila siku mnamwonyesha udikteta, hata naye anataka muda wa kufanya kazi,” akasema Bw Wandayi. Alikuwa akiongea baada ya kuzuru eneobunge la Turbo Kaunti ya Uasin Gishu ambayo ni ngome ya kisiasa ya Rais Ruto. Bw Wandayi aliwaambia viongozi wa upinzani wakome kukosoa Rais Ruto na kuwachochea Wakenya dhidi ya utawala wake. Badala yake aliwataka wawe na subira hadi 2027 wakati ambapo Wakenya wataelekea debeni. “Maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika hayana chochote kuhusiana na Gen Z ila ni mbinu ya wanasiasa wenye umero wasiokuwa na subira wanaotaka mamlaka kwa mlango wa nyuma. Rais Ruto ni kama marais wengine na lazima ahudumu na kukamilisha muhula wake,” akaongeza Bw Wandayi. Waziri huyo alisema anaunga mkono Rais Ruto na yupo tayari kupambana na wanasiasa ambao wanapinga utawala wake huku akionyesha imani kiongozi wa nchi atachaguliwa tena 2027. “Kama wameamua kumsumbua Rais Ruto nasi pia tutamlinda na kumtetea ili afanye kazi yake, amalize muhula wake na kwa mapenzi ya mwenyezi Mungu awahi muhula mwingine,” akaongeza Bw Wandayi. Waziri huyo pia alifuchua kuwa mpango upo wa kusambaza umeme kwa nyumba zaidi Uasin Gishu upo baada ya kaunti hiyo kutengewa Sh1.8 bilioni katika mwaka huu wa kifedha. “Turbo pekee yake imepokea Sh200 milioni ili kuunganisha umeme na serikali ya kaunti itaongeza Sh75 nyingine kuhakikisha umeme upo nyumba zote,” akasema Bw Wandayi.
from Taifa Leo https://ift.tt/v0hbp8c
via
IFTTT