Uchanganuzi: Kila serikali imekuwa na ‘mbwa’ haramu wa kuwinda wapinzani

SERIKALI ya sasa imemulikwa kwa kutumia kikosi haramu cha polisi kuwatesa wapinzani, mtindo ambao unaonekana kuigwa kutoka kwa tawala za nyuma zilizolaumiwa kuendeleza ukatili huo.

Alipochukua usukani mnamo Septemba 13, 2022, Rais William Ruto aliahidi kuwa utawala wake haungevumilia vikosi haramu vya polisi kama kile spesheli kilichobuniwa kutokana na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ambacho kilikuwepo alipohudumu kama naibu wa rais chini ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Mauaji ya kiholela lazima yakome, ni haramu, hayafuati katiba na yanavuruga haki ya kuishi,” Rais Ruto alisema alipokutana na viongozi wa Mamlaka Kuu ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA).

Hata hivyo, kauli hiyo imeonekana kuwa maneno matupu baada ya madai kusambaa kuwa kuna kikosi cha siri cha DCI kinachowalenga wapinzani wa Rais Ruto.

Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, kabla ya kuondoka nchini mnamo Julai 9 kuelekea Amerika, alidai kuwa alifahamu kikosi cha siri katika Idara ya Ujasusi (NIS) ambacho kilihusika katika utekaji nyara na mauaji ya waliokuwa wakiandamana kwa amani.

Bw Gachagua alidai kikosi hicho kinachofahamika kama 101 kilikuwa cha wanaume ambao walihusika na uharibifu na uporaji wa mali wakati wa maandamano.

Alidai kuwa kikosi hicho kiliundwa alipokuwa serikalini na kilikuwa kimepewa mafunzo ya juu kukabiliana na maasi.

Serikali, hata hivyo ilikanusha uwepo wa kikosi cha polisi kinachoua watu kiholela licha ya Bw Gachagua kusisitiza kuwa kipo na lazima kivunjwe.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alisisitiza kuwa polisi wote wanafanya kazi chini ya sheria na oparesheni zote hufanyika kwa kuzingatia sheria.

“Iwapo afisa yeyote wa polisi atashutumiwa kwa kutumia nguvu kinyume cha sheria, basi sheria hiyo hiyo itamwaandama,” akasema Bw Murkomen akimjibu Bw Gachagua Jumanne wiki iliyopita.

Hata hivyo, kila utawala nchini umekuwa ukijipata pabaya, ukilaumiwa kwa kutumia kikosi cha siri kisichofuata sheria na kuwaangamiza wapinzani.

Katika enzi za Rais Daniel arap Moi (1978-2002), kulikuwa na kikosi maalum cha Special Branch ambacho kwa sasa kilibadilishwa jina na kuitwa NIS.

Kikosi hicho kilikashifiwa kwa kukiuka haki za binadamu na mauaji ya kiholela.

Enzi za Rais Mwai Kibaki, vikosi vilivyofahamika kama Eagle, Flying Squad na kile kikali zaidi cha Kwekwe vilikuwa vikiendesha shughuli zao kimasomaso na kupuuza sheria huku vikilaumiwa kwa mauaji na mateso.

Ni enzi hizo za utawala wa Kibaki ambapo kikosi cha Kwekwe kilishutumiwa kwa kuwaua mamia ya vijana ambao walishukiwa kuwa wanachama wa Munguki.

Wakati wa utawala wa Uhuru Kenyatta na naibu wake Ruto, kulikuwa na kikosi maalum cha DCI maarufu kama Special Service Unit (SSU) ambacho kilivunjwa na Rais Ruto alipotwaa mamlaka 2022.

Ni kikosi hicho cha SSU kilichohusishwa na kupotea kwa raia wa India Zulfiqar Ahmad Khan na Mohamed Zaid Sami Kidwa ambao walikuwa katika jopo la kampeni za Rais Ruto.

Rais Ruto aliamrisha maafisa wa usalama ambao walihusishwa na kutoweka kwa wanaume na derava wao wa teksi Nicodemus Mwania, washtakiwe kwa mauaji.

SSU pia kilitajwa kuhusika katika mauaji ya vijana waliotupwa katika Mto Yala.

Kukanusha uwepo wa kikosi hicho cha siri katika serikali ya Rais Ruto kulizua maswali mnamo Julai mwaka jana wakati wa maandamano ya Gen-Z waliokuwa wakipinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Taifa Leo iliripoti kuwa kulikuwa na kikosi kilichokuwa kimeshirikisha maafisa wa NIS na DCI ambacho kilikuwa kimeundwa kupambana na maandamano ya Gen-Z.



from Taifa Leo https://ift.tt/TGqPcSY
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post