Upinzani sasa warai Magharibi watimue Ruto, Raila 2027

VIONGOZI wa upinzani waliendeleza ziara yao katika eneo la Magharibi mwa Kenya huku wakihimiza wakazi wa eneo hilo kumkataa Rais William Ruto pamoja na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, katika uchaguzi wa 2027. Walitoa wito kwa wakazi wa eneo la Magharibi, ambako Bw Odinga amekuwa akipata uungwaji mkono kwa wingi katika chaguzi zilizopita, kuungana ili kumuondoa Dkt Ruto mamlakani 2027, na kumtaka kuanza kuandaa mizigo yake kuondoka Ikulu “wakati Wakenya watamkataa kupitia kura.” Kiongozi wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, na aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, walisema kuwa hali ya wananchi mashinani inaonyesha chuki kubwa dhidi ya utawala wa Dkt Ruto. “Tumekuwa tukizunguka kote nchini tukisikiliza maoni ya wananchi na wengi wanasema wazi kuwa Ruto ni rais wa muhula mmoja tu. Hasira dhidi ya serikali yake inazidi kupanda,” alisema Bw Gachagua. Alisema Wakenya wamechoshwa na utawala wa Rais Ruto ambao umejawa na ukatili, utekaji nyara, mauaji, na watu kutoweka kwa lazima, hasa wale wanaompinga, huku ushuru wa juu ukisababisha mateso ya kiuchumi kwa wananchi. Kiongozi huyo wa chama cha DCP alimshutumu Rais Ruto kwa kuendeleza ukabila, akisema kuwa utawala wake ni kikwazo kikubwa kwa mshikamano wa kitaifa na maendeleo. “Tumekuwa Pwani, Ukambani, kwa Wamaasai na sasa hapa Magharibi na sauti za wananchi ni zile zile – kila mtu anasema Ruto lazima aondoke. Hana chaguo bali kujiandaa kuondoka,” alisema Bw Gachagua akiwa Mumias, siku ya pili ya ziara yao. Alisema upinzani utawashirikisha vijana wa kizazi cha Gen Z kusimamia uchaguzi wa 2027, kuhakikisha hakutakuwa na wizi wa kura. “Hatutategemea IEBC kwa matokeo. Tutakuwa na vituo vyetu vya kujumlisha kura kwa sababu maafisa wa IEBC ni wafuasi wa Ruto,” aliongeza. Kwa mujibu wa Bw Gachagua, siasa ni mchezo wa idadi na Rais Ruto anazidi kupoteza idadi ya wafuasi kila uchao. Alisema tayari Dkt Ruto amepoteza kura milioni nne alizopata kutoka eneo la Mlima Kenya baada ya wao kutalikiana kisiasa kupitia mchakato wa kumtimua madarakani. “Nawaomba radhi Wakenya kwa kumsaidia Ruto kuwa Rais. Nilimsaidia kwa njia nyingi, lakini sasa nitawasaidia Wakenya waliokandamizwa kumpeleka nyumbani,” aliongeza. Kikosi hicho kilizunguka maeneo mbalimbali kuanzia Mumias hadi soko la Ogalo na Butula huko Busia, mji wa Bungoma, Chwele, Kimilili, Kiminini hadi Kitale. Bw Musyoka alimtaka Rais Ruto kuwashukuru viongozi wa upinzani kwa kumruhusu kumaliza muhula mmoja. “Vijana wa Gen Z walikuwa na nia ya kumaliza muhula wake ukiwa nusu tu. Tumempa muhula mmoja hadi 2027 na anapaswa kushukuru kwa hisani hiyo. Tunataka ifikapo 2027, akubali uamuzi wa Wakenya na kuondoka Ikulu bila vurugu yoyote,” alisema Bw Kalonzo. Bw Musyoka alisema kuwa ingawa Bw Odinga amekuwa akipata kura nyingi kutoka eneo la Magharibi, hakuna miradi yoyote ya maendeleo aliyoanzisha katika eneo hilo. “Nimefanya kazi na Raila Odinga katika chaguzi tatu zilizopita na nikaona anapata kura nyingi kutoka huku. Lakini yeye hukita maendeleo tu katika eneo lake la Nyanza,” alisema. Aliyekuwa waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, aliwataka vijana wawe makini na maandamano, akisema serikali ina nia ya kuwamaliza vijana hao wakati wa maandamano. Naibu kiongozi wa chama cha DCP, Bw Cleophas Malala, alisema alifanya kampeni kali kuhakikisha Dkt Ruto alipata kura nyingi zaidi Kakamega, lakini alifukuzwa serikalini. “Ninawashauri, msiamini kila anachowaambia Ruto. Ana maneno matamu lakini ni mjanja sana. Hata barabara alizozindua zamani akiwa Naibu Rais hazijakamilika. Ni mwerevu sana na anapaswa kukataliwa 2027,” alisema Bw Malala. Kiongozi wa chama cha DAP-K, Bw Eugene Wamalwa, alisema kuwa vijana 134 waliuawa wakati wa maandamano chini ya utawala wa Rais Ruto. “Katika maandamano ya mwaka 2023, vijana 75 waliuawa, 61 mwaka 2024 na tumepoteza 18 katika maandamano ya hivi karibuni. Mauaji haya ya vijana wanaotumia haki yao ya kidemokrasia lazima yakome kwa kumwondoa Ruto 2027,” alisema Bw Wamalwa.

from Taifa Leo https://ift.tt/h7oaTMO
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post