
HATUA ya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kuendelea kushambulia ushirikiano kati ya kiongozi wa chama hicho Raila Odinga na Rais William Ruto imeibua mjadala kuhusu mipango ya chama hicho kuelekea 2027. Kwa upande mmoja seneta huyo wa Nairobi imejisawiri kama mwaasi anayelenga kuvuruga ODM kutoka ndani huku upande mwingine akionekana kama anayetumiwa na Bw Odinga kuendeleza mikakati yake ya kujiondoa kutoka mkataba kati ya ODM na UDA. Huku Bw Odinga akishikilia kuwa ushirikiano kati yake na Rais Ruto utadumishwa hadi 2027, Bw Sifuna amekuwa akipinga msimamo huo akisema ni “mbaya zaidi.” Hali hiyo imewashangaza maadui na wandani wa chama hicho cha Chungwa wasijue nani kati ya Bw Odinga na Bw Sifuna anapasa kuaminiwa. Seneta Sifuna amekuwa akiikosoa Serikali Jumuishi, inayoshirikisha wanachama watano wa ODM wanaoshikilia nyadhifa za uwaziri, kwa ukatili wa polisi na mauaji ya kiholela miongoni mwa dhuluma nyinginezo. Katibu huyo Mkuu amekuwa akishikilia kuwa ODM haiko serikalini na haitamuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. Nyakati nyingine, Bw Sifuna amekuwa akipiga waziwazi kauli za kiongozi wa chama chake. “Ushirikiano wetu na serikali ya Kenya Kwanza unatugharimu pakubwa. Unatuumiza kama chama kwa sababu upande wake Rais haujajitolea kutekeleza yale tuliyokubaliana kwenye mkataba wa ushirikiano na ndio maana ninasema umekufa,” akasema Bw Sifuna. “Nataka Ruto ajue kwamba kuondolewa kwake afisini ni ajenda kuu ya kitaifa. Ndio ajenda ya kipekee kwa sababu serikali yake inapinga maadili yaliyoorodheshwa kwenye Katiba. Kwa mtazamo wangu ninaunga mkono kuondolewa kwa Ruto. Hoja ya kumtimua afisini ikiwasilishwa katika seneti, nitaiunga mkono haraka zaidi,” akaongeza. Seneta huyo wa Nairobi alieleza kuwa uamuzi wa kushirikiana na UDA ulifikiwa kuzuia kuporomoka kwa taifa la Kenya baada ya maasi ya vijana wa Gen Z Juni mwaka jana. Lakini, kulingana na Bw Sifuna, ODM haifai kudumisha ushirikiano huo hadi 2027 kwa sababu UDA imedinda kutekeleza MOU hiyo iliyotiwa saini Machi 7, mwaka huu. Alieleza kuwa aliishauri ODM dhidi ya kutia saini mkataba wa ushirikiano na UDA kwani hatua hiyo ingefuta masuala ambayo ODM imekuwa ikitetea, lakini ushauri wake ulikataliwa. Wakati wa mahojiano ya kipekee na NTV nyumbani kwake mtaa wa Karen, Nairobi, Jumamosi, Bw Odinga alisema uamuzi wa ODM kushirikiana na utawala wa Rais Ruto ulifanywa kwa ajili ya kudumisha uthabiti wa kitaifa. Alieleza kuwa ushirikiano huo ulifikiwa kufuatia msururu wa maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na Gen Z mwaka kiasi cha kulitumbukiza taifa hili katika lindi la machafuko sawa na hali ilivyo Somalia, Haiti au Sudan. “Tumesema kuwa tuko katika serikali jumuishi hadi mwaka wa 2027. Hatukusema kuwa tutafanyakazi na UDA hadi baada ya 2027. Hayo ni masuala ambayo yatajadiliwa wakati ufaao na uamuzi kufanya na wanachama wa ODM sio Raila kama mtu binafsi,” akaeleza Bw Odinga. Lakini kwa upande wake, Katibu Mkuu, Sifuna, anashikilia kuwa ODM ikidumisha ushirikiano wake na utawala huu hadi 2027, haitapata nafasi ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu. Hali hii, akasema, itaikosesha ODM nafasi ya kujiondoa kutoka kwa serikali iliyopoteza umaarufu na kuelezea wananchi sababu ya kushirikiana na utawala huo. “Kwa hivyo sielewi ni kwa nini baadhi ya wenzetu wanaona ni bora kuendelea kushirikiana na serikali hii hadi 2027 kinyume na matakwa ya wanachama wengi,” akaeleza Bw Sifuna.
from Taifa Leo https://ift.tt/Ld9i5fb
via
IFTTT