Walijitokeza kusaidia, lakini miaka miwili baadaye, madhila bado yanawasumbua. Iliacha alama akilini mwao, wakisumbuliwa na ndoto mbaya, maono ya miili iliyooza, na mateso ya kiakili ambayo hata pombe haiwezi kuyazima usiku unapoingia.
Walikuwa waendeshaji wa boda boda wa kawaida, vijana wa miaka ya ishirini, waliokuwa wamezoea vumbi na mashimo ya barabara za vijijini Kaunti ya Kilifi, si wahudumu wa mochari wala waokoaji wa dharura waliobobea.
Machi 2023, serikali ilipoomba msaada wa kutafuta na kuondoa miili kutoka makaburi ya pamoja msituni Shakahola, waliitikia wito. Wafu hao walikuwa wafuasi wa mhubiri tata Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International.
Kwa miezi kadhaa, kwa ujasiri waliendelea kuchimba makaburi ya kina kifupi msituni na kutoa zaidi ya miili 450 iliyooza, wakiwemo watoto, ambao wengi hawakutambulika.
Kile kilichoanza kama wito wa huduma, kiligeuka kuwa jinamizi lisiloisha. Miaka miwili baadaye, vijana hao wanakiri kubeba makovu ya kisaikolojia. Wanaendelea kuteseka na ndoto mbaya, kumbukumbu za miili iliyooza, na msongo wa mawazo unaowaandama kila siku.
Wakati wengine walioshiriki moja kwa moja au kwa njia nyingine katika shughuli hiyo wanapoonekana kusonga mbele, kundi hili limeachwa nyuma, limesahaulika.
Hawakupoteza jamaa zao katika janga hilo, lakini athari za kiakili za shughuli ya mwaka mzima zimevuruga maisha yao.
Ingawa walilipwa posho ya kila siku wakati wa oparesheni hiyo, gharama ya kweli imekuwa makovu ya kudumu katika afya yao ya akili.
Wao huitwa kwa kejeli “wachimbaji wa makaburi wa Mackenzie.” Ni jambo ambalo hawapendi kulizungumzia. Baada ya mazungumzo marefu kuhusu umuhimu wa hadithi yao, walikubali kuzungumza, ingawa walijua hatukuwa na msaada wa moja kwa moja wa kisaikolojia.
Salim Charo alifanya mtihani wa KCSE mwaka wa 2022 na alikuwa na ndoto ya kujiunga na chuo. Wakati mauaji ya Shakahola yalipotokea, alikuwa akilima ili kupata karo ya masomo.
Asubuhi moja Machi, taarifa za watu waliodhoofika kiafya kupatikana msituni zilienea kijijini. Viongozi waliomba vijana wajitolee kusaidia katika uokoaji.
“Ndivyo nilivyojikuta msituni. Uokoaji uligeuka kuwa kazi ya kuchimba makaburi. Tulianza kutoa mifupa,” anasema.
Alidhani angehusika kwa siku chache tu, kisha arudi shambani. Hakutarajia kushiriki awamu zote tano za uchimbaji.
Posho ya Sh1,000 kwa siku na ahadi ya serikali kuwapatia kazi baadaye vilimpa motisha kuendelea.
“Wakati mwingine ningetoa hadi miili 12 kutoka kaburi moja. Kazi yangu ilikuwa kuchimba na kuvuta miili, mara nyingi ikiwa imefungwa kwa blanketi au mifuko myeupe ya plastiki,” anasema kwa huzuni.
Lakini baada ya kazi kuisha, kumbukumbu hazikufutika.
“Siwezi kulala. Nikilala naota wafu wananikimbiza. Wanaonekana bado wako hai. Nikiamka siwezi lala tena,” asema.
Aliwaona watu waliokuwa wamepoteza nguvu wakiwa hai, na wengine walifariki baadaye. Walikuwa wateja wa Madukani waliokuwa wakija kununua chakula.
Mshtuko huo ulimgharimu hata uhusiano wake wa kimapenzi.
“Mpenzi wangu aliniacha. Aliniambia mimi na wengine ni wachimbaji wa makaburi wa Shakahola. Akaondoka,” asema. Analaumu ushauri duni wa kisaikolojia uliotolewa na serikali.
Anasema ushauria ulikuwa mfupi na ulifanywa kwa kikundi, badala ya kila mmoja kushauriwa binafsi.
“Tulitoka kuchimba makaburi, tukasikiza ushauri kwa dakika chache kisha tukarudi tena kazini asubuhi. Haikuwa na maana. Mara ya mwisho nilihudhuria ushauri ilikuwa Julai 23, 2023.”
“Najihisi nikiwa nimetumika na kutelekezwa. Walipaswa kutoa usaidizi zaidi wa kisaikolojia na kutimiza ahadi ya ajira.”
Emmanuel Ngolo aliacha kazi ya boda boda na sasa anasaidia kwenye shamba la baba yake.
“Wateja walipoanza kunihusisha na makaburi, walianza kuniepuka. Wangechukua pikipiki ya mwingine. Wapinzani walitunyanyapaa,” asema.
Jefa Juma anasema bado anakumbuka harufu ya maiti. “Harufu ile bado ipo puani mwangu.”
Aliacha kucheza mpira kwa sababu ya kejeli.
“Wakati wa mechi, wapinzani walitucheka.Tukishindwa, waliniambia ni mkosi wa makaburini.”
Stephen Safari anaamini ndiye aliyetowa miili mingi zaidi. Anasemekana kuwa na matatizo ya akili kutokana na yale aliyoshuhudia msituni.
Aliwahi kuwa fundi ujenzi, lakini aliacha kutokana na majeraha aliyopata msituni.
Dkt Frank Njenga, mtaalamu wa magonjwa ya akili, anakubali kuwa dalili kama ndoto mbaya ni athari za tukio kama hilo.
“Ndiyo hali kamili ya tukio kama hili. Ni hali ya kiakili inayojitokeza baada ya mshtuko mkubwa,” asema.
Anaeleza kuwa hali hii inaweza kujitokeza hata miezi sita baada ya tukio na wengine huathirika baada ya muda mrefu zaidi.
“Kila mtu huathirika tofauti kulingana na hali ya awali ya afya ya akili. Wale waliokuwa na matatizo ya awali huhitaji usaidizi wa kina zaidi.”
from Taifa Leo https://ift.tt/ceXolQH
via IFTTT