Washirika wa Gachagua waingia baridi, waogopa kujiuzulu

WANDANI wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wanaonekana kupuuza wito wake wa kuwataka wajiuzulu nyadhifa zao za ubunge na kutetea viti vyao kwa tiketi ya chama chake kipya - Democracy and Citizen’s Party (DCP). Mnamo Februari mwaka huu, Bw Gachagua alitangaza kuwa wandani wae walikuwa akisubiri uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kisha wajiuzulu kutoka chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto. Mpango huo, kulingana na Bw Gachagua, ulinuiwa kulazimisha “uchaguzi mkuu mdogo” haswa katika eneo la Mlima Kenya kuthibitisha kuwa ushawishi wa UDA eneo hilo umeisha kabisa na wakazi wote wamejiunga na chama kipya cha DCP. “Tumeamua kusubiri uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC kisha tuzindue chama chetu. Tutakuwa na chaguzi nyingi ndogo. Kufikia sasa kuna madiwano 139 wanaosubiri kujiuzulu kutoka UDA na wajiwasilishe kwa chaguzi ndogo,” Bw Gachagua akasema mnamo February 24, 2025. “Tunalazimisha uchaguzi mkuu mdogo baada ya uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC kwa sababu watu wetu hawataki kuishi katika uwongo. Watu wa Mlima Kenya wanapenda ukweli, ni watu wenye maadili na hawataki kujidanganya,” akasema Bw Gachagua. Aliendelea na kuwataka madiwani, wabunge na maseneta wandani wake “kufanya uamuzi wa kibusara” huku akiwahakikishia kuwa watachaguliwa upya. Bw Gachagua aliwahakikisha wandani wake ambao wangediriki kujiuzulu na kujitokeza kwa uchaguzi mdogo kwa tiketi ya DCP akiwahakikisha kuwa watachukuliwa kama “mashujaa” na siasa yao itanawiri. Lakini baada ya chama chao chake cha DCP kuzinduliwa na makamishna wapya wa IEBC kuchaguliwa, wandani wa Bw Gachagua sasa wanajivuta, hawataki kujiuzulu. Baadhi ya wale tuliowahoji walisema kuwa suala hilo, la kujiuzulu, halijawahi kujadiliwa katika chama hicho kipya. Baadhi yao walisema kuwa suala ambalo wanalipa kipaumbele wakati huu ni chaguzi ndogo zilizochangiwa na vifo vya wabunge na baadhi yao kuteuliwa kuwa mawaziri. Mbunge wa Gatanga Edward Muriu alisema ingawa mpango huo ungalipo, sio suala linalopewa kipaumbele katika chama cha DCP wakati huu. “Kwanza tunataka kujishughulisha na chaguzi ndogo zilizoko. Tunataka kuhakikisha chama cha DCP kinashinda viti vyote vitakavyoshindaniwa katika eneo la Mlima Kenya. Mambo mengine yatakuja baadaye,” akasema Bw Muriu. “Lakini ifahamike kuwa bado ajenda yetu ni kuondoa Mlima Kenya kutoka kwa UDA iliyowasaliti watu wetu,” akasema. Kwa upande wake, Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru almaarufu Mejjadonk, uamuzi kuhusu kujiuzulu UDA utafanywa na wabunge kama watu binafsi. Alisema hamna msimamo wa chama kwamba wabunge wote waliochaguliwa kwa tiketi ya UDA wajiuzulu na kuwania upya kwa tiketi ya DCP.

from Taifa Leo https://ift.tt/XzFjinQ
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post