Bodaboda watakiwa wawe balozi wa amani na ‘kitulizo’ kwa Gen Z

WAHUDUMU wa bodaboda wametakiwa waeneze amani na umoja ili kuwatuliza vijana baada ya taifa kushuhudia maandamano ya Gen Z. Wazungumzaji katika tamasha la amani eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado, walisema vijana wanastahili kudumisha amani na kutumia idadi yao kujipanga kwa kura ya 2027 badala ya kushiriki ghasia na maandamano. Tamasha hiyo ilihudhuriwa na wahudumu wa bodaboda zaidi ya 1300, viongozi wa kidini na wananchi. Ngong’, Ongáta Rongai, Kitengela, Kiserian ni kati ya miji kwenye Kaunti ya Kajiado ambayo ilishuhudia wimbi kali la maandamano ambalo liliwaacha baadhi ya vijana wakiwa wameaga dunia na uharibifu mkubwa wa mali ya umma. Kwenye baadhi ya matukio, ilidaiwa maandamano hayo yalikuwa yameingiliwa na wahuni waliokuwa kwenye bodaboda. Wakati wa tamasha hiyo ya amani wahudumu wa bodaboda waliraiwa wawe kiungo cha amani na wajizuie kutumika wakati wa ghasia. Mwenyekiti wa Muungano wa Wahudumu wa Bodaboda Kaunti ya Kajiado Alex Gitari alisema kuwa watashirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha kuna amani mijini na mashinani wanapoendelea na kazi yao ya kusaka riziki. “Katika maandamano ya hapo awali, wanachama wetu wameshuhudia jinsi ambavyo ghasia zinaweza kuathiri namna wanavyopata riziki. Tunawataka wanachama wetu wawe watu wa kueneza amani kila wakati,” akasema Bw Gitari. Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kajiado Kaskazini Tom Achia aliwataka raia na wahudumu wa boda boda wawachukulie maafisa wa usalama kama ndugu na dada zao badala ya adui ili kuwe na mnato wa kueneza amani. “Polisi sio maadui wa umma bali ni ndugu na dada zetu ambao wanahusika na kulinda mali ya umma jinsi ambavyo imenakiliwa kwenye katiba yetu,” akasema Bw Achia. Mhubiri Lucy Wangunjiri kutoka Kanisa la PBB, ambalo liliandaa tamasha hiyo ya amani, aliwataka wamakinikie amani badala ya kukubali kugawanywa kwa msingi wa kisiasa. “Vijana wengi wanapata riziki kupitia boda boda. Hii ni kazi nzuri ambayo inafanya familia kadhaa kujikimu na hatufai kuichezea kwa kuingiza uhuni,” akasema Kasisi Wangunjiri.

from Taifa Leo https://ift.tt/J3Swf1T
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post