VIGOGO wa kisiasa wanapambana kudhibiti kaunti ya Nairobi vyama vyao vikimezea mate kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, wote wamezindua kampeni ya kuwavutia wapiga kura zaidi ya milioni mbili wa kaunti ya jiji.
Kwa mujibu wa data ya IEBC, Nairobi ilikuwa na wapiga kura wengi zaidi nchini, 2,415,310, katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Wachambuzi wa kisiasa wanasisitiza kwa msingi huu wa kuwa na wapiga kura wengi, pamoja na umuhimu wake kama kitovu cha uchumi, Nairobi ni muhimu kwa muungano wowote wenye ndoto ya kushinda urais mnamo 2027.
“Nairobi si kaunti tu; ni alama ya nguvu ya taifa,” anasema Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia University of Kenya. Mrengo wowote ukidhibiti Nairobi, unatoa ishara kali kwa nchi nzima kuhusu nguvu zake kisiasa.”
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, Johnson Sakaja alishinda kiti cha ugavana kwa tiketi ya UDA, akimshinda Polycarp Igathe wa Jubilee aliyeungwa na Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga katika muungano wa A zimio.
Sakaja alipata kura 699,392 (asilimia 54.95) dhidi ya Igathe aliyepata 573,516 (asilimia 45.06) ushindi ulioonyesha ukuaji wa ushawishi wa Kenya Kwanza katika jiji kuu.
Kabla ya uchaguzi huo, Odinga alilazimika kupata Igathe kama mgombea wa ugavana wa Nairobi wa muungano wa Azimio na hivyo kuondoa mgombea wa ODM, Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi, jambo lililozua malalamishi ndani ya ODM kaunti ya Nairobi.
Sasa, miaka miwili kabla ya uchaguzi wa 2027, kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi kimeanza kushika kasi na kinatarajiwa kuwa mojawapo ya zenye ushindani mkali zaidi nchini.
Wanasiasa wakuu wanaopigwa darubini katika mapambano hayo ni Rais Ruto na Raila Odinga katika serikali jumuishi dhidi ya Gachagua na Kalonzo Musyoka wa Wiper wote wakipanga kuwa na mgombeaji wa ugavana kujenga ushawishi katika mji mkuu.
Sakaja amesema mafanikio yake ya muhula wa kwanza ndio msingi wake wa kuwania muhula wa pili tena.
Wanyonyi, aliyeonekana kama mpinzani mkuu wa Sakaja, amejiondoa na kuelezea azima ya kugombea ugavana Bungoma, akitegemea makubaliano ya awali kati ya Rais Ruto, Raila, na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya.
Ingawa wapinzani wapo wengi kama Mbunge Babu Owino (Embakasi East), Mbunge James Gakuya (Embakasi North), mwanahabari wa zamani Tony Gachoka, na Irungu Nyakera ( wa chama chaDCP) bado ushindani ni mkali. Wengine waliotajwa ni Dennis Waweru, Agnes Kagure, George Aladwa, na Ferdinand Waititu, ambaye majuzi alipata dhamana kuondoka gerezani anakotumikia kifungo kwa ufisadi
Babu Owino tayari ametangaza nia yake ya kugombea hata bila tiketi ya ODM akidai kuwa ndiye mgombea bora. Gachoka pia ametangaza nia yake kwa tiketi ya KANU akisema ana nguvu ya kutosha kumshinda Sakaja.
Nyakera amejiunga na chama cha DCP cha Gachagua kumenyania tiketi na Gakuya.
Sakaja, licha ya uhusiano wake na UDA, ameendelea kuwa na uhusiano mzuri na Rais Ruto na Raila Odinga, jambo linaloongeza uvumi kuhusu uwezekano wa kuungwa na viongozi hao wawili.
Tafsiri: BENSON MATHEKAfrom Taifa Leo https://ift.tt/k2A0G8B
via IFTTT