Wakazi washtaki mbunge kwa kujenga shule mpya bila idhini yao

WAKAZI 30 wa Kaunti ya Mandera wamemshtaki mbunge kwa kujenga shule ya sekondari kwa siri bila kuhusisha umma au kuomba maoni yao.

Mbunge wa Mandera Kusini Haro Abdul Ebrahim, ameshtakiwa na wakazi hao wa eneobunge la Kotulo kwa madai ya kuwadhalilisha na kuwanyima watoto wao haki ya kupata elimu bora kwa kushindwa kuboresha shule zilizopo.

Badala yake, Ebrahim anadaiwa kutumia vibaya fedha za umma kwa kuajiri mkandarasi kujenga shule mpya ya sekondari karibu na shule iliyopo, ambayo inahitaji ukarabati mkubwa.

Katika kesi iliyowasilishwa mahakamani kwa dharura na wakili Pauline Kiteng’e, wakazi hao wanaomba Mahakama Kuu kusimamisha ujenzi wa shule hiyo mpya iitwayo Gode Secondary School, iliyo umbali wa hatua chache kutoka Borehole Eleven Mixed Secondary, eneo la Borehole Eleven.

Wapinzani wa mradi huo wameeleza Mahakama Kuu kuwa mbunge wao Ebrahim aliwaajiri wanakandarasi kwa siri kujenga shule hiyo mpya bila kushauriana na wakazi wa eneo hilo, jambo ambalo ni ukiukaji wa haki zao za kimsingi na kinyume na Ibara ya 10 ya Katiba ya Kenya.

Wakazi hao, wakiongozwa na Abdia Abdula Hassan, wametaja Bodi ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge ya Serikali Kuu (NG-CDF) na mbunge Ebrahim kama washtakiwa katika kesi hiyo.

Pia, wametaja Wizara ya Elimu ikiongozwa na Waziri Julius Migos Ogamba, Bodi ya Elimu ya Kaunti ya Mandera, Kamishna wa Kaunti, na Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti-ndogo ya Kutulo kama wahusika wa ziada katika kesi hiyo.

Wakazi hao wamedai kuwa haki zao zimekiukwa na Ebrahim pamoja na NG-CDF, kwa kuwa "watoto wao wamekosa haki ya kupata elimu ya msingi, huku haki yao ya kushirikishwa kwenye maamuzi ya maendeleo ya umma ikipuuzwa."

"Mshtakiwa wa pili, Ebrahim, anaendelea kukiuka haki za wakazi wake, na vitendo vyake vinatishia kuvuruga amani ya jamii, na kwa hivyo tunaomba Mahakama Kuu iingilie kati haraka," alisema Wakili Kiteng’e katika stakabadhi zilizowasilishwa kortini.

Wakili huyo pia anaomba Mahakama Kuu iitambue kesi hiyo kuwa ya dharura, na itoe amri ya muda ya kusitisha ujenzi wa shule ya Gode, hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Zaidi ya hayo, Kiteng’e anaomba mahakama iagize NG-CDF na Mbunge Ebrahim kubomoa jengo la shule hiyo linalojengwa kwa siri karibu na shule ya Borehole Eleven.



from Taifa Leo https://ift.tt/tjkO6a4
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post