MFUMO mpya unaowahitaji maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kulipia chakula hautaathiri wanajeshi wote, Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya amefafanua mbele ya wabunge.
Waziri huyo jana aliambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi kwamba wanajeshi wanaohudumu shughuli za kulinda amani nchi za ng’ambo, wanaoshiriki operesheni maalum na wale wanaohudhuria mafunzo hawataathiriwa na sera hiyo.
Kulingana na Bi Tuya, watakaoathiriwa na sera hiyo mpya, iliyoanza kutekelezwa kuanzia Julai 1, 2025, ni wanajeshi wanaohudumu katika maeneo salama pekee.
“Kumekuwa na malalamishi kule nje na watu wengine wameingiza siasa katika suala hili. Tumia nafasi hii kutoa maelezo kamili kuhusu namna sera hiyo itatekelezwa,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Nelson Koech.
Alipoulizwa na wabunge ikiwa umma ulipewa nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu sera hii mpya, Bi Tuya alisema wadau wote walishirikishwa ‘kindani’ kabla ya utekelezaji wake kuanza.
Kamati hiyo inataka Wizara ya Ulinzi kuwasilisha ripoti kuhusu shughuli ya ushirikishaji wa umma iliyoendesha kuthibitisha kuwa wadau-wanajeshi- waliidhinisha sera hiyo alivyodai Bi Tuya.
“Sera ya kulipia chakula iliyoanzishwa na wizara yangu sio geni. Imekuwepo. Imechukua mahala pa sera ya chakula kisicholipiwa. Ushirikishaji wa umma ulifanywa kindani,” Bi Tuya akasema.
Suala hilo liliibuliwa na Mbunge wa Kajiado ya Kati Memusi Kanchori aliyeitaka Waziri kutoa ufafanuzi kuhusu sera hiyo akisema madai ya kupotosha yamekuwa yakitolewa kuhusu suala hilo.
“Inaendeshwa vipi? Je, inawavunja moyo wanajeshi wetu?” Bw Kanchori akauliza.
Bi Tuya alikana madai kuwa sera hiyo inawavunja moyo wanajeshi akisema inawafaidi kwa sababu imechangia kuongezwa kwa marupurupu yao.
“Haiwavunji moyo wanajeshi wetu. Waathiriwa pekee ni wanajeshi wanaohudumu katika maeneo salama. Wanajeshi wanaohudumu katika maeneo hatari na wale wanaopokea mafunzo bado wanafurahia mpango wa lishe bila malipo,” Bi Tuya akasema.
Chini ya mfumo huu mpya, wanajeshi wanahitaji kulipia chakula chao, kwa pesa taslim au makato kutoka kwa mishahara yao.
Kubadilishwa kwa sera ya chakula kunasemekana kulenga kupunguza ubadhirifu wa pesa za umma na kuhakikisha kuimarisha ufanisi katika huduma ya utoaji lishe katika KDF.
from Taifa Leo https://ift.tt/Sf2Cpi3
via IFTTT