
SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, ametetea Bunge dhidi ya lawama kwamba inachelewesha kutungwa kwa sheria ya kuwatimua wabunge, akisema kuwa wanasubiri Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwasilisha Mswada husika kujadiliwa. Katika mahojiano ya kipekee na
Taifa Leo, Bw Wetang’ula alisema kuwa baada ya baadhi ya vipengele vya Sheria ya Uchaguzi ya 2011 kuhusiana na utaratibu wa kuwatimua wabunge kufutwa na mahakama, jukumu la kuandaa sheria mpya ni la IEBC na Mwanasheria Mkuu. “Sheria yoyote kuhusu kuwatimua wabunge haijawahi kuwasilishwa bungeni na kukataliwa. Ni nani anayefaa kuileta? Nafikiri mamlaka sahihi ya kuandika na kuwasilisha mswada huo ni IEBC,” alisema Bw Wetang’ula. Aliongeza kuwa akiletewa mswada huo bungeni, atahakikisha unapitishwa kwa haraka kwa kufuata taratibu zote za sheria, “Kuna madai kuwa kuna ombi la kumtimua mbunge mmoja, na watu wanadai hakuna sheria ya kufanya hivyo. Sasa jukumu ni la IEBC na Mwanasheria Mkuu kukaa chini, kuandaa rasimu ya sheria hiyo, kisha kuileta bungeni ndipo watu waanze kulaumu Bunge iwapo itachelewesha,” aliongeza Bw Wetang’ula. “Kwa hivyo Bunge halina hatia yoyote katika kuchelewesha sheria hiyo. Na sidhani kuna mbunge yeyote ambaye atapendekeza mswada wa kuondolewa kwake mwenyewe. Ni hali ya mwanadamu,” alisema. Kifungu cha 104 cha Katiba kinaelekeza kuwa Bunge litapitisha sheria itakayoweka misingi ya kumuondoa mbunge katika wadhifa wake na taratibu zitakazofuatwa. Wiki iliyopita, IEBC ilisema kuwa Bunge bado halijarekebisha Sheria ya Uchaguzi kufuatia uamuzi wa mahakama, na kwa hivyo hakuna sheria inayoweza kutumika kwa sasa kuwatimua wabunge. Mnamo 2017, jopo la majaji watatu – Kanyi Kimondo, George Odunga na Chacha Mwita – lilitangaza vipengele kadhaa vya sheria ya kuwatimua wabunge kuwa vya kibaguzi, visivyo na maana na kinyume cha Katiba. Bw Wetang’ula alisisitiza kuwa si Bunge lililokwenda kortini kupinga sheria hiyo. “Si ni wananchi wenyewe waliokwenda kortini?” aliuliza. Kuhusu uchaguzi mdogo unaosubiriwa katika maeneo bunge sita, Bw Wetang’ula alisema tayari ametoa hati zote muhimu kwa IEBC. “Baada ya siku 21 kwa kila kiti kilichoachwa wazi – kwa kujiunga na serikali au kwa kifo – nilitoa hati ya kukitangaza wazi kwa IEBC kama inavyotakiwa kisheria. Kwa bahati mbaya muda wake ulikwisha bila uchaguzi kufanyika kwa sababu ambazo kila mtu anazielewa,” alisema. Alisema sheria haielezi ni nini kinafaa kufanyika iwapo muda wa hati hizo utakwisha bila uchaguzi kufanyika. “Hakuna kipengele cha kutolewa tena hati hizo. Kwa hivyo tumejadiliana na timu ya sheria ya Bunge, na wiki hii tutaiandikia IEBC kuifahamisha kwamba tuliwahi kutoa hati hizo lakini muda wake ukapita bila uchaguzi kufanyika. Sasa mko kazini, tunataka muanze mara moja maandalizi ya uchaguzi mdogo,” alisema. Bw Wetang’ula alifichua kuwa ameshtakiwa mara kadhaa na wapiga kura wa maeneo yaliyoathiriwa kwa madai ya kukosa uwakilishi bungeni. “Kama Spika, nikishatoa hati, mimi si sehemu tena ya mchakato huo. Kwa hivyo kunishtaki ni upuuzi wa hali ya juu ambao mtu atalazimika kujieleza kortini,” alisema. TAFSIRI: BENSON MATHEKA
from Taifa Leo https://ift.tt/q3omO8D
via
IFTTT