UKUZAJI wa mikonge ni shughuli inayohitaji maandalizi mazuri ya shamba, uteuzi wa miche bora, na uvumilivu kwa sababu zao hili ni la kudumu na hukaa shambani kwa zaidi ya miaka kumi.
Mchakato huanza kwa kuandaa shamba. Eneo huchaguliwa liwe na udongo wenye mifereji mizuri ya maji na usio na maji kusimama.
Mikonge hustawi vizuri zaidi katika maeneo ya ukanda wa Pwani na nyanda za chini zenye mvua ya wastani, hali inayopatikana kwa wingi katika mikoa ya Tanga na Morogoro nchini Tanzania, na pia sehemu za Kibwezi na Kilifi nchini Kenya.
Shamba hulimwa na magugu kuondolewa, mashimo huchimbwa kwa nafasi za wastani wa mita moja kati ya mmea mmoja na mwingine, ili kuruhusu mimea kukua vizuri bila kuathiriana. Baada ya shamba kuandaliwa, miche ya mikonge hupandwa.
Miche hii kwa kawaida hutokana na vichipukizi vinavyotolewa kwenye shina la mmea mama.
Vichipukizi hivi huchaguliwa kwa makini ili kuhakikisha vina afya njema na havina magonjwa. Upandaji hufanyika mwanzoni mwa msimu wa mvua ili miche iweze kushika mizizi vizuri.
Baada ya kupandwa, hufuata hatua ya matunzo ya mimea. Mikonge haihitaji mbolea nyingi, lakini mara nyingine huwekewa mboji ili kuimarisha ukuaji.
Shamba huendelea kudhibitiwa magugu, hasa katika miaka ya mwanzo ambapo mimea bado huwa michanga.
Mikonge inajulikana kwa kustahimili ukame, jambo linalofanya iwe rahisi kukuzwa katika maeneo kame ya Kenya na Tanzania.
Baada ya miaka mitatu hadi minne, mmea wa mikonge huanza kutoa majani makubwa yenye nyuzi. Katika hatua hii, mavuno huanza.
Uvunaji hufanywa kwa kung’oa majani ya nje, huku yale ya ndani yakiachwa ili mmea uendelee kukua.
Majani hukatwa kwa mikono kwa kutumia panga kali na huchukuliwa hadi kiwandani.
Kiwandani, nyuzi hutolewa kwa njia ya kuchakata (decortication). Mashine maalum hutenganisha nyuzi kutoka kwenye jani.
Baada ya nyuzi kutolewa, hukaushwa kwa jua, kisha kuchambuliwa kulingana na ubora.
Nyuzi safi na zilizo bora zaidi hutumiwa kutengeneza bidhaa za viwandani, ilhali nyuzi za kawaida hutumiwa kutengeneza kamba na bidhaa nyinginezo za matumizi ya kawaida.
Baada ya kila mavuno, mmea huendelea kutoa majani mapya. Mikonge inaweza kuzaa kwa zaidi ya miaka kumi kabla ya zao hilo kung’olewa.
Baada ya hapo, shamba hupumzishwa au kupandwa upya. Kwa ujumla, mchakato wa ukuzaji wa mikonge unahusisha maandalizi ya shamba, upandaji wa miche, matunzo, uvunaji wa majani, uchakataji wa nyuzi kisha uuzaji wa bidhaa.
Nchini Tanzania na Kenya, hatua hizi zimetumika kwa miongo mingi na zimeendelea kubadilika kadri teknolojia mpya inavyoibuka.
from Taifa Leo https://ift.tt/zuIQ9EW
via IFTTT