Huzuni baba, mwanawe wakizama baharini

SAFARI ya uvuvi ya baba na mwanawe kisiwani Lamu iliishia kwa mkasa baada ya mashua yao kupinduka katika Bahari Hindi.

Famau Bwanahamadi, 78, amekuwa akifanya kazi ya uvuvi pamoja na mwanawe Hassan Famau, 27, kwa miaka mingi kutoka Lamu hadi Malindi katika Kaunti ya Kilifi na maeneo mengine ya Pwani.

Bwanahamadi anatambulika kama mvuvi mkongwe zaidi aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kote Lamu.

Jumatatu, wawili hao walirekebisha nyavu zao kabla kuelekea eneo la Pezali karibu na Kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki, kwa kutumia mashua yao ya Sima Kuu.

Kulingana na familia, Bwanahamadi na mwanawe kwa kawaida huingia baharini jioni, kuvua usiku kucha na kurejea nyumbani asubuhi ya siku inayofuata.

Walipokosa kurudi nyumbani kufikia saa sita mchana Jumanne familia na marafiki waliingiwa na wasiwasi wakapiga ripoti mara moja kwa ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Nchini (KMA) zilizoko Lamu.

Bw Bunu Vae, binamu ya Bwanahamadi, alisema uzoefu na uvumilivu wa marehemu katika kazi yake ya uvuvi uliwafanya wengi wamchukulie kama shujaa wa sekta hiyo.

“Wavuvi wengi chipukizi Lamu wamejifunza mengi kutokana na mbinu za Bwanahamadi. Hii iliwawezesha kuwa vile walivyo leo. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” alisema Bw Vae.

[caption id="attachment_178390" align="alignnone" width="2560"] Kikosi cha majanga na uokozi cha kaunti ya Lamu kikiwasili eneo la jeti ya hospitali ya King Fahd kisiwani Lamu Alhamisi Septemba 25, 2025 kuufikisha mwili wa mvuvi, Hassan Famau, 27. Mwili huo uliopolewa kutoka kwa Bahari Hindi eneo la Kwa Adi-Taudhi, karibu na Bandari ya Lamu huko Kililana.
PICHA|KALUME KAZUNGU[/caption]

Taarifa za kutoweka kwa wawili hao zilisambazwa kwa mashirika yanayoshughulika na majanga ya baharini, ikiwemo Shirika la Huduma za Ulinzi wa Pwani Nchini (KCGS), Shirika la Red Cross na Kitengo cha Kukabiliana na Majanga cha Kaunti ya Lamu.

Operesheni ya pamoja ya uokoaji ilianzishwa mara moja, na mwili wa Bwanahamadi ukapatikana ukielea baharini karibu na Mtangawanda mnamo Jumanne jioni.

Zoezi hilo liliendelea Jumatano na jana. Ni jana mchana ambapo waokoaji walipata mwili wa Hassan katika eneo la Kwa Adi-Taudhi karibu na Bandari ya Lamu.

Mashua waliyoitumia haikuwa imepatikana. Inakisiwa chombo hicho cha uvuvi walichokuwa wakitumia kilizidiwa nguvu na upepo mkali pamoja na mawimbi, na kupinduka.

Mkasa huo unaaminika kutokea Jumatatu usiku walipokuwa wakivua samaki katika eneo la Pezali.

Akithibitisha kisa hicho meneja wa Kituo cha Dharura cha Kaunti ya Lamu (EOC), Bw Ifakhar Majid, alisema miili hiyo ilisafirishwa hadi hospitali ya King Fahd mjini Lamu.

Kulingana na kiongozi wa kikosi cha uokoaji cha Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Musa, operesheni ilichukua muda mrefu kwa sababu ya mawimbi makali baharini.

Mkurugenzi wa KMA Kanda ya Kaskazini, Bw Alexander Munga, alihimiza wavuvi na watumiaji wengine wa bahari kuvaa fulana maalum za kuelea majini kila wanapokuwa baharini.

[caption id="attachment_178391" align="alignnone" width="2560"] Afisa anayeongoza kikosi cha Majanga na Uokozi Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Musa. Asema operesheni ilitatizwa na mawimbi makali na dhoruba baharini. PICHA|KALUME KAZUNGU[/caption]

Diwani wa Mkomani Abbas Shekhuna, alisikitika kuwa wavuvi wengi wanalazimika kuingia hadi katika bahari kuu bila vifaa vya kisasa.

Alitoa wito kwa serikali kuharakisha awamu ya pili ya fidia ya wavuvi walioathiriwa na mradi wa ujenzi wa bandari ya Lamu; awamu inayojumuisha kuwapa vifaa vya kisasa ili kuboresha usalama.

Mwenyekiti wa muungano wa vyama vya usimamizi wa fuo za Lamu, Bw Mohamed Somo, alilalamikia ongezeko la visa vya wavuvi kupoteza maisha baharini katika siku za hivi majuzi.

Bw Somo alisema katika muda wa chini ya miezi miwili tayari wamepoteza wavuvi wasiopungua watano.

Kauli yake iliungwa mkono na Katibu wa Chama cha Usimamizi wa Ufuo wa Lamu Abubakar Twalib, ambaye aliongeza kwamba wavuvi wanakabiliana na changamoto si haba ikiwemo uvuvi haramu unaoendeshwa na vyombo vya kigeni, ukosefu wa rasilimali na umasikini unaosukuma wengi kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kupata riziki.



from Taifa Leo https://ift.tt/q1b8GUs
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post