Nina siri ya kushinda ugavana Nairobi bila Raila, Babu Owino asema

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino amemlaumu Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa masaibu yake ya kisiasa huku akisema kuwa sasa anajipanga kivyake kuhusiana na azma yake ya ugavana wa Nairobi mnamo 2027.

Bw Owino ametaja kitendo cha Bw Odinga kumkinga Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja dhidi ya kungólewa na madiwani mapema mwezi huu kama ishara tosha kuwa hana nafasi ya kupewa tikiti ya ugavana na ODM 2027.

“Inashangaza wakati wa vita Babu alikuwa akihitajika na bado nakumbuka vyema jinsi tulivyomiminiwa risasi na Baba (Raila) na Junet (Mbunge wa Suna Mashariki). Sasa hakuna mtu ananijali na hata kama kuna makombo yanayoanguka afadhali yafagiliwe badala ya Babu kupata,” akasema Bw Owino.

Akionekana kuwa mwenye machungu na majuto kwa kuhangaikia ODM, Bw Owino ambaye alikuwa akiongea na Idhaa ya Nam Lolwe inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiluo, alisema mambo yake na ODM yameisha na apewe au akose kupokezwa tikiti, bado ana siri kali ya kuhakikisha anamshinda Bw Sakaja debeni.

“Mungu ambaye alinitoa Nyalenda Kisumu kutoka kwa umaskini mkubwa, akanifanya nikawa kiongozi wa wanafunzi mara nne na kisha mbunge mchapakazi kwa mihula miwili, ndiye atanipa ugavana Nairobi licha ya wengine kuidhinishwa,” akasema.

Mwanasiasa huyo alifichua kuwa masaibu yake yalianza wakati ambapo maombi yaliandaliwa mnamo Februari 10 ambapo Bw Odinga alikuwa akiwania kiti cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Ni katika maombi haya ambapo Bw Odinga na baadhi ya viongozi wa ODM walimuidhinisha Bw Sakaja awanie kiti cha ugavana.

“Hayo maombi yalikuwa feki na yalikuwa yamepangwa ili kuniabisha. Hata hivyo, nilifahamishwa kilichokuwa kikiendelea na nikageuka kisha kurudi nyumbani,” akaongeza.

Bw Owino hasa alishangaa kwa nini Bw Odinga aliamua kuwashawishi madiwani wa ODM wasiendelee na mpango wa kumtimua Bw Sakaja uongozini.

Mnamo Septemba 2, ilichukua juhudi za Bw Odinga na na Rais William Ruto kuwashawishi madiwani zaidi ya 90 ambao walikuwa wametia saini hoja ya kumtimua Bw Sakaja afisini.

“Sote tulimwona Raila akimwokoa Sakaja ambaye utendakazi wake ni duni na hata madiwani wanahiari kujiuzulu kwa sababu wadi zao hazipati maendeleo. Hata ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali zimeonyesha jinsi kaunti inatumia vibaya pesa za umma,” akasema Bw Owino.

Mbunge huyo, alishangaa kwa nini sasa Bw Odinga na uongozi wa ODM umempa mgongo ilhali alikuwa mtu wa kwanza kunyakwa na kuzuiliwa kwa siku tatu punde tu utawala wa sasa ulipoingia mamlakani.

Tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na kampuni zimemwonyesha Bw Owino akiwa kifua mbele japo anasema kuwa ana umaarufu na siri ya kuhakikisha ndiye gavana wa Nairobi 2027.



from Taifa Leo https://ift.tt/cEbNnBQ
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post