Pwagu apata pwaguzi mteja akipata agizo auze mali ya benki

Familia ya aliyekuwa wakati mmoja Waziri, Mbiyu Koinange, imepokea idhini ya mahakama kupiga mnada mali ya Ecobank Kenya Limited ili kufidia deni la Sh840 milioni, linalotokana na utoaji haramu wa fedha kutoka kwa akaunti ya marehemu takriban miaka 15 iliyopita na watu waliokuwa wakihusika katika kesi ya urithi.

Kulingana na hati za mahakama, kiasi hicho kinajumuisha Sh284 milioni kama fedha za msingi zilizotolewa kutoka kwa akaunti mnamo 2011, na riba ya Sh556.6 milioni.

Uamuzi huo unaashiria hatua nyingine katika mzozo wa kisheria uliodumu kwa miongo minne kuhusu mali ya marehemu Koinange inayokadiriwa kuwa ya thamani ya Sh14 bilioni, ambapo mahakama iliagiza kampuni ya madalali ya Moran Auctioneers kutwaa mali ya benki hiyo ili kulipa deni hilo.

Hati ya kuruhusu kuuzwa kwa mali mnadani ilitolewa Ijumaa na Msajili Msaidizi wa Idara ya Familia katika Mahakama Kuu ya Milimani, ikimuagiza dalali kupiga mnada mali ya benki hiyo.

Dalali huyo pia ameagizwa kuwasilisha hati hiyo tena kortini kufikia Novemba 18, 2025, akieleza jinsi alivyoitekeleza au sababu za kutoitekeleza.Hati hiyo ilitolewa chini ya Kesi ya Urithi Na. 527 ya 1981, baada ya benki hiyo kushindwa kutii uamuzi wa Juni 26, 2025 wa Jaji Eric Ogolla, aliyeagiza benki hiyo irudishe Sh284 milioni pamoja na riba.

Jaji Ogolla alipata benki hiyo kuwa na uzembe wa makusudi kwa kuruhusu kutolewa kwa fedha kutoka kwa akaunti ya urithi iliyo chini ya ulinzi wa mahakama, kinyume na agizo la mahakama.

Jaji alisema benki hiyo ilichukulia akaunti hiyo kwa uzembe kwa kuruhusu kutolewa kwa pesa hizo licha ya agizo la mahakama la mwaka 2011 lililozima matumizi yoyote bila idhini.

Mjane wa Koinange, Bi Eddah Wanjiru, mmoja wa wasimamizi wa mali hiyo, aliomba mahakama kuamuru kurejeshwa kwa fedha hizo akisema zilikuwa zimehifadhiwa katika akaunti hiyo kufuatia agizo la mahakama la Julai 26, 2011.



from Taifa Leo https://ift.tt/mBvkXzL
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post