Raila agutuka, aanza kulinda gome zake

KIONGOZI wa chama cha ODM Raila Odinga ameanza kulinda ngome zake za kisiasa dhidi ya uwezekano wa kuvamiwa na mshirika wake Rais William Ruto.

Bw Odinga ameanza harakati kali za kukifufua chama chake huku akionya hadharani wandani wake dhidi ya kuunga mkono azma ya Rais Ruto ya kuchaguliwa tena 2027.

Akiwa na changamoto za migawanyiko ya ndani na kuibuka kwa makundi ya kisiasa, Waziri Mkuu huyo wa zamani amelazimika kurejesha ushawishi wake wa kisiasa, huku kukiwa na hofu kwamba ushirikiano wake mpya na Rais Ruto unaweza kudhoofisha chama chake cha ODM kilicho na historia ya miaka 20.

Bw Odinga ameanzisha shughuli mbalimbali za kisiasa ili kufufua matawi ya chama chake mashinani na kulinda ngome zake za jadi.

Shughuli hizi ni maandalizi ya maadhimisho ya miaka 20 ya chama hicho yatakayofanyika mwezi ujao katika kaunti za Mombasa na Kilifi.

Tayari chama hicho kimeandaa mikutano mikuu ya hadhara katika kaunti za Kisii, Wajir na Narok. Pia kimefanya chaguzi za mashinani kuanzia vituo vya kupigia kura hadi kiwango cha kaunti, kabla ya Mkutano Mkuu wa Kitaifa (NDC) unaopangwa kufanyika Machi 2026.

Kukiwa na minong’ono kuwa ODM huenda ikaingia kwenye mkataba wa kisiasa na chama tawala cha UDA kuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027, Bw Odinga anataka kuhakikisha kuwa hakuna uvamizi katika ngome za jadi za chama hicho.

Chama hicho kinajitahidi kuhakikisha kuwa kinadumisha ushawishi wake mkubwa katika maeneo ya Nyanza, Magharibi na Pwani. Viongozi wa ndani ya chama wanaamini kuwa ni kwa kudumisha ngome hizi ndipo Bw Odinga ataweza kuwa na nafasi ya maana katika serikali ijayo.

“Hatujapitisha azimio lolote kusema jinsi tutakavyoshiriki uchaguzi wa 2027. Kwa hivyo popote ulipo, usikiuke msimamo wa chama kwa mambo ambayo hayajajadiliwa,” alisema Bw Odinga.

“Wacha mambo hayo yajadiliwe kwanza. Sisi ni ODM. Nani aliwaambia ODM haitakuwa na mgombea 2027? Fikiria kwanza kama ODM. Tuna mpango ambao tumejadiliana na kukubaliana. Maamuzi mengine yatafanywa wakati ufaao,” aliongeza.

Kauli hizo zilitolewa wakati wa mkutano wa wabunge wa ODM jijini Machakos wiki iliyopita.

Haya yanajiri wakati ambapo baadhi ya viongozi wa ODM, wakiwemo waliowahi kuwa maafisa wa juu wa chama na sasa wako serikalini, wametangaza hadharani kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.

Rais Ruto alishinda uchaguzi wa 2022 kwa msaada mkubwa wa maeneo ya Bonde la Ufa na Mlima Kenya. Hata hivyo, Mlima Kenya—uliompa kura karibu milioni tatu—unaonekana kusambaratika baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kuondolewa mamlakani. Hii inamweka Rais katika hatari ya kisiasa na kumsukuma kutafuta maeneo mapya ya kura.

Rais ameanza kulenga ngome za ODM kwa matumaini ya kutumia uhusiano mpya na mpinzani wake wa zamani, Bw Odinga.

Lakini, kwa kutotaka kuachwa mikono mitupu iwapo mwelekeo wa kisiasa utabadilika, Bw Odinga ameanza kampeni mashinani, na wiki iliyopita alizuru Wajir na Kisii ambapo alisisitiza kuwa ODM inalenga kushinda uchaguzi wa 2027, peke yake au kwa kushirikiana na vyama vingine vyenye malengo yanayofanana.

“Tutahakikisha kuwa ODM inaunda serikali ijayo, ama iwe sehemu ya serikali hiyo. ODM haitaitwa tena chama cha upinzani,” alisema Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohamed.

“Sisi kama ODM, kiongozi wetu ni Raila Odinga. Yeye ndiye tunamfuata, akisema twende kushoto, tunaenda kushoto,” akaongeza Mwenyekiti wa chama hicho, Bi Gladys Wanga.

Jumapili, wandani wa Bw Odinga walikuwa Narok kujenga uungwaji mkono wa chama hicho. Ujumbe huo uliongozwa na Bi Wanga, aliyekuwa ameandamana na Bw Mohamed, naibu mwenyekiti wa chama Godfrey Osotsi (Seneta wa Vihiga), Seneta wa Narok Ledama Ole Kina miongoni mwa wengine.

“Jamii ya Wamaasai imekuwa nguzo ya chama cha ODM kwa miaka mingi, wakichangia kueneza misingi ya chama chetu,” alisema Bi Wanga.

Alisema kuwa chama bado kimejipanga kushika hatamu ya uongozi, iwe kama chama pekee au kwa ushirikiano. Alitaja mapambano ya chama kwa haki ya kijamii, ugatuzi na heshima kwa haki za binadamu kama baadhi ya maadili ambayo yamefanya ODM kudumu kwa miaka 20.

“Tumekuwa thabiti kwa kile tunachosimamia. Kiongozi wetu amekuwa jasiri na mwaminifu. Ndiye aliyekuwa kiunganishi; ndio maana ODM ina wanachama kote nchini,” alisema Bi Wanga.

Chama hicho kimepanga maadhimisho ya siku tatu kati ya Oktoba 10 hadi 12, 2025 yatakayofanyika Mombasa na Kilifi kusherehekea miaka 20 ya chama hicho.



from Taifa Leo https://ift.tt/9ByP3RT
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post