Nema yatathmini ombi la kujenga jaa la kuzika taka zenye sumu kali za ‘asbestos’ Kilifi

MAMLAKA ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) imepokea ripoti ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) kuhusu mradi unaopendekezwa wa ujenzi wa jaa la kutupa taka za 'asbestos' katika eneo la Kalumani/Mnyenzeni, Kaunti ya Kilifi.

Mradi huo unaosimamiwa na kampuni ya Asbe Contractors Limited unalenga kujenga jaa maalumu lenye ua na mashimo ya kuzika taka za asbestos.

Kwa mujibu wa NEMA, kampuni hiyo inalenga kuweka mfumo salama wa utupaji wa taka hizo hatari ambazo zinaathiri mazingira na afya ya binadamu endapo hazitashughulikiwa kwa njia sahihi.

Wananchi walipewa siku 30 kuanzia Ijumaa iliyopita kutoa maoni yao kwa NEMA kuhusu mpango huo.

Asbestos ni aina ya paa zilizotengenezwa kwa madini hatari ambayo yalitumiwa kwa wingi zamani katika sekta ya ujenzi.

Mbali na paa, zilitumiwa pia kujenga mabomba na sakafu, kutokana na uwezo wake wa kustahimili moto na kemikali.

Hata hivyo, tafiti za kiafya zimeonyesha kuwa, kuvuta hewa yenye chembechembe za asbestos kunaweza kusababisha magonjwa hatari kama vile saratani ya mapafu, au kuvimba kwa mapafu.

Itakumbukwa kuwa, miezi michache iliyopita, serikali iliagiza mipango iwekwe ili asbestos ziondolewe kwa majengo yote ambayo bado yana paa au sehemu nyingine zilizotengenezwa kwa vifaa aina hiyo.

Hata hivyo, mdahalo uliibuka kuhusu jinsi hatua hiyo itachukuliwa bila kudhuru afya.

Ili kupunguza athari hizi, NEMA ilisema ripoti ya EIA imependekeza kuwa, eneo litakalojengwa jaa hilo kuwe na mashimo ya taka ambayo yatafunikwa kwa plastiki na kisha kufungwa kwa chombo cha saruji ili kuzuia kuvuja kwa chembechembe zozote za asbestos.

Aidha, wafanyakazi wote watakaohusika na uondoaji na utupaji wa taka za asbestos watapewa mafunzo maalum kuhusu hatari zinazotokana nazo na mbinu salama za kushughulikia.

Watapewa pia vifaa vya kujikinga kama mavazi maalum, glovu na viatu, ambavyo vitatumiwa mara moja tu na kutupwa pamoja na taka za asbestos.

Eneo la taka litabandikwa mabango ya onyo, na mpango wa dharura utawekwa tayari kukabili matukio yoyote ya ajali au kuvuja kwa chembechembe.

Wafanyakazi hao pia watapimwa kiafya mara kwa mara ili kufuatilia athari zozote zinazoweza kujitokeza.

Taka zote zenye uchafu wa asbestos, pamoja na udongo au vifaa vingine vilivyochafuliwa wakati wa usafishaji, zitazikwa ndani ya jaa hilo.

Taka za kawaida zitagawanywa kulingana na aina na kushughulikiwa na kampuni iliyopewa leseni na NEMA.



from Taifa Leo https://ift.tt/vOftWVE
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post