Biashara zakadiria hasara Mombasa licha ya utulivu wakati wa maandamano

LICHA ya Kaunti ya Mombasa kushuhudia utulivu waandamanaji walipojitokeza barabarani katika kaunti nyingine 17 mnamo Jumatatu, bado uliwagharimu wafanyabiashara wa jiji hilo. Jumanne asubuhi, wamiliki wa biashara walikuwa wanakadiria hasara walizopata wakati wa maadhimisho ya Saba Saba kwa hofu ya uharibifu, huku wachache waliokuwa wamefungua wakifichua kuwa walipata hasara au kuuza bidhaa chache mno siku nzima. Wafanyabiashara kadha waliokuwa wameweka vyuma au mbao kufunika madirisha yao ya vioo, walilazimika kugharamika tena kuziondoa Jumanne. Bw Kennedy Mumbo, mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Baa Mombasa, alisema maeneo mengi ya burudani yalikuwa yamefungwa licha ya kuwa hakukuwa na maandamano yoyote. “Kila mtu alikuwa na hofu akitarajia jambo fulani kutokea. Wengi waliamua kufunga biashara zao ili kupunguza gharama za uendeshaji na hata waliokuwa wamefungua, hawakuwa na wateja,” alisema Bw Mumbo. Aliongeza, “Utalii unastawi mahali ambapo kuna amani na ndiyo maana tunatoa wito wa mashauriano ili kupunguza hali ya wasiwasi inayoshuhudiwa nchini kwa sasa.” Katika Mkahawa wa Sandrus ulio katikati mwa jiji la Mombasa, mmiliki wake, Bw Yahya Baradhia, alisema walifanikiwa kuuza theluthi moja tu ya mauzo yao ya kawaida, na hivyo kupata hasara kubwa. “Kwa vile huwa tuna wateja wengi wa kila siku, tuliamua kufungua, lakini tulipata hasara kwa kuwa wateja wetu wa kawaida hawakuagiza, kwani ofisi nyingi zilikuwa zimefungwa. Tulibaki na chakula kingi ambacho hakikuuzwa, na hatupaswi kusahau gharama ya kuwalipa wafanyakazi wetu waliokuwa na kazi kidogo sana,” alilalamika. Katika saluni ya Mintos ambako vijana karibu 15 wameajiriwa, mmiliki aliamua kufunga biashara hiyo ili kuepuka hasara na kulinda maisha. “Wafanyakazi wetu ni wa kudumu na tunapaswa kuwalipa hata kama hawakufanya kazi, lakini mji ulikuwa mtupu,” alisema Bw Tony Mintos, mmiliki wa saluni hiyo. Maduka mengi, yakiwemo ya magari, shule na ofisi zilikuwa zimefungwa Mombasa mnamo Jumatatu ingawa hakukuwa na maandamano. Wachache waliokuwa wamefungua biashara zao walikuwa waangalifu sana, wakiwa tayari kufunga ghafla iwapo kungetokea ghasia zozote. Hali ya usafiri haikutatizwa, ingawa kulikuwa na abiria wachache sana waliokuwa wakiingia na kutoka katikati ya jiji. Hii ilifanya kuwe na magari machache ya uchukuzi wa umma na pia ya kibinafsi barabarani, na hivyo kusababisha hasara pia kwa sekta ya uchukuzi, mafuta na kwa serikali ya kaunti ambayo hutoza ada za uegeshaji kila siku. Wauzaji bidhaa katika masoko kama vile Marikiti na Kongowea pia walikadiria hasara, kwani wateja wengi hawakuenda kununua bidhaa. Kwa jumla, hakukuwa na maandamano katika kaunti zote za Pwani zinazojumuisha Lamu, Kilifi, Kwale, Taita Taveta, Tana River mbali na Mombasa. Hata hivyo, tofauti na Mombasa ambapo wakazi wengi walibaki mitaani wakihofia usalama wao, hali ya kawaida ilishuhudiwa katika kaunti hizo nyingine ambapo shughuli ziliendelezwa kama kawaida.

from Taifa Leo https://ift.tt/Ahn92kQ
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post