
MAELEZO mapya yameibuka kuhusu jinsi uporaji na vurugu za Jumatatu zilivyopangwa na kutekelezwa katika eneo la Mlima Kenya, ambapo polisi na wafanyabiashara wanasema kulikuwa na taarifa za kijasusi mapema kwamba biashara fulani zilikuwa zimetambuliwa na kulengwa kwa uporaji. Walihojiwa pia walidai kuwa wahuni walilipwa, kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ya eneo hilo ambapo walitishia usalama, wakielekezwa na 'amri kutoka juu'. Hii ilitokea huku viongozi wakirushiana lawama kuhusu nani aliyehusika kulipa wahuni walivamia na kupora biashara wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya Siku ya Saba Saba. Kamanda wa Polisi wa Imenti Kaskazini, Bw Ambrose Kyalo, alisema kuwa waporaji waliopenya maandamano ya Saba Saba walikuwa na malengo na maagizo maalum. Hadi sasa, polisi wamewakamata watu 60 katika Kaunti ya Meru, wanaoshukiwa kupanga uporaji huo. “Washukiwa wanachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na watafikishwa mahakamani hivi karibuni. Uchunguzi wa awali unaonyesha waporaji waliovamia biashara walikuwa na maagizo maalum na waliratibiwa vizuri ili kukwepa polisi. Walikuwa wakilenga Kiwanda cha Meru Dairy, maduka ya maalum ya jumla, vituo vya polisi na mabohari ya Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao,” alisema Bw Kyalo. Katika mji wa Nyeri, biashara angalau 10 ziliharibiwa huku wahuni wakikabiliana na polisi siku nzima. Maduka yaliyolengwa ni pamoja na maduka ya mavazi, mikahawa, baa, maduka ya simu, na maduka ya rejareja. Wavamizi waligeukia biashara hizo baada ya kushindwa kuingia katika maduka makubwa mjini humo. Kaunti ya Murang’a ilipokea taarifa za kijasusi kuwa maandamano zaidi yanapangwa kufanyika Julai 11, 2025, wakati wa mazishi ya marehemu Boniface Kariuki. Bw Kariuki, mchuuzi jijini Nairobi, alipigwa risasi na polisi alipokuwa akiuza barakoa mnamo Julai 25, 2025, na alifariki wiki mbili baadaye.
from Taifa Leo https://ift.tt/NMvHwuZ
via
IFTTT