Tafuteni mbinu nyingine ya kukosoa serikali lakini si fujo, Kindiki aambia upinzani

NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki amewarai Wakenya na viongozi kutafuta mbinu mbadala na ya amani ili kutatua shida za kitaifa badala ya vurugu, maandamano na Saba Saba.

Akihutubia umma eneo la Mkunguni kisiwani Lamu Jumatatu, Prof Kindiki alishikilia kuwa ni jambo la busara kwa viongozi na wananchi kuipenda nchi yao na kuhakikisha tofauti zilizoko zinatatuliwa kwa njia ya mazungumzo na amani.

Prof Kindiki aiyazungumza hayo wakati alipoongoza hafla ya mchango wa fedha kwa makundi ya wanawake na vijana kisiwani humo.

Naibu huyo wa Rais alishikilia kuwa haitawezekana kujenga nchi ya Kenya kupitia vita na vurumai za kila mara, hatua aliyoitaja kuhatarisha amani, umoja na usalama wa kitaifa.

Alisema ni haki ya kikatiba kwa wananchi kuwa na maoni tofauti kuuhusu uongozi au serikali.

“Wale wenye maoni tofauti kuhusu serikali, mko na haki kufanya hivyo kikatiba ila lazima yote yatendeke kwa njia ya amani. Najua mnakubaliana na mimi wenzangu kwamba hakuna kitu cha thamani katika taifa au ulimwengu kuliko usalama na amani,” akasema Prof Kindiki.

Aliwakashifu wale wanaopanga vita na vurugu za kila mara nchi, akionya kwamba kufanya hivyo siyo njia ya kujenga bali ni kubomoa taifa tukufu la Kenya.

Prof Kindiki aidha aliendelea kumpigia debe Rais William Ruto kuweza kuchaguliwa tena kwa awamu ya pili ifikapo Uchaguzi Mkuu wa 2027, akitaja maendeleo mengi aliyofikisha Lamu, Pwani na Kenya kwa jumla kwamba yanamruhusu kuendelea kuiongoza nchi.

“Tunasema Ruto kumi bila breki. Ukiangalia hapa Lamu serikali kupitia Rais Ruto imetenga Sh307 milioni kuunganisha nyumba kwa stima. Kuna maegesho ya uvuvi Mokowe yanayojengwa kwa kima cha Sh239 milioni. Ukitazama eneo la Lamu Mashariki limepata barabara ya lami inayoendelea kwa mara ya kwanza tangu uhuru. Mambo mengine mengi yanatekelezwa hapa Lamu na Kenya kwa jumla. Tumuunge mkono Rais wetu kwa kipindi cha pili,” akasema Prof Kindiki.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula aliushutumu upande wa upinzani unaoongozwa na Naibu wa zamani wa Rais, Rigathi Gachagua kwa kukosa ajenda.

Bw Wetangula alisema inashangaza kwamba ajenda walizonazo wapinzani zote zinahusu ‘Ruto Aende,’ ‘Ruto Awamu Moja,’ ‘Kasongo’ nakadhalika.

“Ukitazama upande wa upinzani hauna ajenda wala sera zozote isipokuwa zile za Kasongo, Ruto Aende nakadhalika. Hizo si ajenda. Wananchi mmakinike na kuepuka hawa viongozi fidhuli,” akasema Bw Wetangula.

Kiongozi wa Wengi Katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah alimkosoa vikali Bw Rigathi Gachagua kwa kuendeleza siasa za chuki na migawanyiko nchini badala ya maendeleo.



from Taifa Leo https://ift.tt/i1tDeMc
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post