Kinaya cha midahalo ya Raila kuanzia BBI, Nadco, Broad-Based sasa Conclave

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga kwa mara nyingine anataka kufanyike Kongamano la Kitaifa la Vizazi Vyote (IGNC) kujadili masuala kama uongozi mbaya, kuzorota kwa uchumi na ukatili wa polisi yanayochochea msururu wa maandamano ya Gen Zs nchini. Hii ni licha ya uwepo wa ripoti kadhaa zenye mapendekezo kuhusu namna ya kushughulikia changamoto, ya hivi punde ikiwa ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco). Yeye na Rais William Ruto ndio waliunda kamati hiyo mnamo Juni 2023 baada ya maandamano yaliyoitiswa na mrengo wake wa Azimio la Umoja-One Kenya kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha, kukithiri kwa ufisadi, madai ya uwepo wa udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa 2022, miongoni mwa malalamishi mengine. Kamati ya Nadco, iliyoongozwa kwa pamoja na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka (akiwakilisha Azimio) na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichungwah (Kenya Kwanz) iliwasilisha ripoti yake mnamo Novemba 23, 2023, kwake (Odinga) na Rais Ruto. Lakini hadi sasa, mapendekezo yake makuu haswa kuhusu namna ya kufufua uchumi ili kupunguza gharama ya maisha na kuzalisha ajira kwa vijana, hayajatekelezwa. Vijana wa Gen Z walipolalamikia changamoto hizo hizo, Juni 2024, kufanya maandamano kote nchi, Bw Odinga alijitokeza na kupendekeza kufanyike mazungumzo mengine kushughulikia matakwa yao kizazi hicho. Lakini wiki chache baadaye alienda kinyume na takwa hilo na kuamua kujiunga na Rais Ruto kuunda serikali jumuishi iliyoshirikisha wandani wake watano katika baraza la mawaziri. Kisingizio chake ilikuwa ni “kuleta utulivu nchini” kufuatia machafuko hayo ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, waandamanaji walivamia majengo ya bunge na kuharibu mali. Sasa, Jumatatu, Julai 7, 2025, baada yake kufeli kuelekea Kamukunji kwa maadhimisho ya Siku ya Saba Saba, Bw Odinga anapendekeza kuundwa kamati nyingine sawa na Nadco, lakini inayoshirikisha vizazi vyote, wakiwemo vijana. “Napendekeza kuundwa haraka Kongamano la Kitaifa la Vizazi Vyote inayowashirikisha vijana, viongozi wa kisiasa, makundi ya kijamii, asasi za kidini na sekta ya kibinafsi kuandaa mkondo mpya kwa taifa hili,” akasema kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi. “Jukwaa hili la mazungumzo sharti lishughulikie malalamishi kuhusu uongozi, kuzorota kwa uchumi, ufisadi na ukatili wa polisi,” akaeleza Bw Odinga, aliyeandamana na wandani wake wa kisiasa, bila kushirikisha vijana. Odinga pia amewahi kushughulikia changamoto hizi hizi, wakati wa muhula wa pili wa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta lakini juhudi zake hazikuzaa matunda.

from Taifa Leo https://ift.tt/fmt7rP2
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post