Mwanasiasa tajika alaumiwa huku waandamanaji watano wakidungwa mishale Kisii

MAADHIMISHO ya Saba Saba yaliingiliwa na wahuni waliovaana na waandamanaji katika Kaunti ya Kisii ambapo majeraha yaliripotiwa.  Zaidi ya waandamanaji watano walijeruhiwa baada ya kudungwa mishale na wahuni hao. Walikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) kwa matibabu lakini wasimamizi wa kituo hicho walikataa kuzungumzia suala hilo. Afisa wa afya anayefanya kazi katika sehemu ya kuwapokea wagonjwa wanaohitaji matibabu spesheli aliambia Taifa Leo kwamba majeruhi walidungwa kwa mishale mikononi. "Tulipokea wagonjwa watano waliokuwa na mishale mikononi mwao. Tulijitahidi kadiri tuwezavyo kuhakikisha kuwa mishale hiyo imetolewa bila kuwadhuru zaidi," alisema afisa huyo aliyeomba jina lake libanwe kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya hospitali hiyo. Waandamanaji waliwanyooshea vidole vya lawama baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo ambao walidai kuwa walisafirisha wahuni ili kutibua maandamano yao ya amani. [caption id="attachment_174598" align="alignnone" width="2560"] Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (KTRH) ambako waandamanaji waliopigwa mshale walikimbizwa kwa matibabu. Picha|Wycliffe Nyaberi[/caption] "Baadhi ya wanasiasa walikodi wahuni na kuwaweka katika maeneo mbali mbali ili kutufuata. Wahuni hao walikimbia kujificha katika majengo yanayositiri afisi za mwanasiasa mmoja kutoka eneo hili. Waandamanaji walipokuwa wakipita karibu na afisi hizo, waliwafyatulia mishale. "Hata hivyo, hilo halitazuia harakati zetu za kupigania utawala bora wa nchi hii," alisema Bw Sammy Nyakundi, mkazi wa Kisii. Vijana walianza kumiminika katika mitaa ya mji wa Kisii mapema kuanzia saa mbili asubuhi. Walianza kwa kuyageuza makutano ya Capital mjini Kisii uwanja wa kuruka kamba, kucheza kandanda na michezo mingine ya kukimbizana. Baadaye, waliwasha moto na kuziba barabara kuu zinazoingia na kutoka Kisii. Polisi walipoona wanaziba barabara hizo, walianza kuwatawanya kwa kuwarushia vitoa machozi. Biashara nyingi zilisalia kufungwa kutwa nzima katika mji huo.

from Taifa Leo https://ift.tt/PGTDKSN
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post