
VIONGOZI wa upinzani jana waliingia mitini siku ya Saba Saba ikiadhimishwa maeneo mbalimbali makabiliano kati ya raia na maafisa wa usalama yakiripotiwa. Hakuna kiongozi wa upinzani hata moja ambaye alijitokeza kwenye maandamano eneo lolote nchini wala hawakuweka wazi shughuli ambazo walikuwa wakishiriki kupitia mitandao ya kijamii. Kuelekea maandamano hayo ya Saba Saba, Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alikuwa amedai kuwa serikali ilikuwa ikiwalenga vijana kutoka Mlima Kenya kwa kuwanyaka kutokana na uharibifu wa mali ambao umekuwa ukishuhudiwa wakati wa maandamano nchini. Akiongea katika mazishi ya shangaziye Kaunti ya Nyeri, Bw Gachagua mnamo Ijumaa alikuwa amesema kuwa hatakubali juhudi za kutenga eneo hilo na kuwanyanyasa vijana aliodai zinaendelezwa na serikali, zifanikiwe. Viongozi wengine wa upinzani Kalonzo Musyoka (Wiper), Eugene Wamalwa (DAP-K) na Dkt Fred Matiang’i pia mitandao yao ya kijamii ilikuwa imekimya. Wanasiasa hao wamekuwa wakisisitiza maandamano ni haki ya Wakenya huku wakitaka serikali iwasikize vijana kutimiza matakwa yao. Vigogo hao wa upinzani wamekuwa na mtindo wa kuitisha kikao na wanahabari baada ya kila maandamano huku hatua hiyo ikiwaletea kejeli kutoka kwa baadhi ya Wakenya. Vijana waliojawa na hamaki walifunga barabara ya Nakuru-Nairobi na kuwasha moto huku shughuli za uchukuzi zikivurugwa kutokana na wimbi la maandamano ya Saba Saba. Polisi walikuwa na wakati mgumu kuwakabili vijana ambao walitumia magurudumu ya magari na mawe makubwa kuziba barabara kuu na hata kuzichoma. Vijana wakiwa wamejihami kwa silaha butu na mawe, waliwarushia mawe polisi katika maeneo ya Free Area, mjini Naivasha na Karai, makabiliano makali yakizuka. Ilibidi polisi watumie gesi za kutoza machozi na kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji hao. Jiji la Nakuru lilikuwa mahame karibu siku yote Jumatatu, wengi wakifunga biashara zao kwa hofu ya kuporwa. Hakukuwa na shughuli zozote za kibiashara kwenye benki, hoteli na maduka ya jumla. Wengi wa wafanyabiashara walifunga kwa sababu waliohofia uporaji ambao ulitokea mnamo Juni 25 ungefanyika tena na kuwasababishia hasara zaidi. Baadhi ya wafanyabiashara hata waliwakodisha vijana waliojihami kwa rungu kuwalindia maeneo yao ya biashara. “Nilikuwa natarajia ningekutana na mteja ambaye ningemtengenezea gari lake lakini hilo halijafanyika kutokana na maandamano haya,” akasema mfanyabiashara Michael Mwangi ambaye ni mekanika eneo la Shabaab. Polisi waliwekwa kulinda asasi za serikali, Ikulu ya Nakuru, Mahakama ya Nakuru na Makao makuu ya Kaunti ya Nakuru. Shule zilifungwa huku magari ya uchukuzi kwenye barabara ya Nakuru-Nairobi, Nakuru-Eldoret, Nakuru-Kabarnet na Nakuru-Nyahururu yakiondolewa kwa hofu ya kuvamiwa. Mjini Naivasha baadhi ya vijana waliziba barabara ya Nairobi-Nakuru Jumapili usiku kuelekea siku ya Saba Saba. Waliwaibia abiria pesa na mali yao. Baadhi ya waendeshaji magari walikumbana na vizingiti hivyo haramu na kulazimika kulipa pesa huku wengine wakivipita kwa kasi. Maeneo yaliyoathirika sana yalikuwa Kayole, Kinungi, Ihindu na Flyover. Polisi waliingilia kati na kuhakikisha kuna utulivu. Naibu Kamanda wa Polisi wa Naivasha Josiah Odongo alisema utulivu ulikuwa umerejea baada ya polisi kufika na kuwatimua wakora waliokuwa wakiwanyanyasa abiria na madereva. “Safari magari yanasonga, hakuna maandamano na tumewafurusha vijana hao,” akasema Bw Odongo. Polisi nao walipambana na waandamanaji kwenye miji ya Nyahururu na Ol Kalou kaunti za Laikipia na Nyandarua. Maeneo hayo yaliathirika sana wakati wa maandamano ya Juni 25 ambapo hata majengo ya serikali yaliteketezwa. Kulikuwa na utulivu kaunti za Bomet na Kericho ambako ni ngome ya Rais William Ruto.
Ripoti za Cecil Odongo, Eric Matara, Mercy Koskei, Waikwa Maina, Vitalis Kimutai, John Njoroge na Tobby Meso
from Taifa Leo https://ift.tt/gaiQlho
via
IFTTT