
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amewaonya wanasiasa anaodai nia yao ni kuendeleza siasa za chuki nchini zinazoweza kutumbukiza taifa hili kwenye ghasia sawa na zilishuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007. Aidha, aliwahimiwa Wakenya kudumisha amani leo, siku ya maadhimisho ya mapambano ya mageuzi ya Saba Saba. Akiongea Jumapili alipohudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la Lord of Promise, Kaunti ya Kwale, Bw Wetang’ula alikariri ya viongozi wa kisiasa kupalilia mshikamano wa kitaifa na heshima kwa haki za raia wote. “Hatuwezi kuruhusu taifa letu kurejeshwa katika enzi za machafuko ya mwaka wa 2007 hadi mapema 2008 ambapo maafa na uharibifu mkubwa wa mali ulitokea,’ akawaambia waumini. Bw Wetang’ula alionekana kurejelea kauli aliyotoa Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mapema mwezi jana alipotisha kuwa ghasia mbaya kuliko zile za baada ya uchaguzi wa 2007 zitatokea nchini endapo serikali ya Kenya Kwanza itashiriki wizi wa kura. “Wakijaribu kuiba kura, ghasia zitakazotokea zitakuwa mbaya zaidi kiasi kwamba zile za 2007 zitaonekana kama karamu ya Krimasi,” Bw Gachagua alisema Juni 2, kwenye mahojiano na tovuti moja. Jana, Spika Wetang’ula aliitaka Kanisa kuwa mstari wa mbele kuhubiri jumbe za kuhimiza na kuendeleza amani na umoja wa kitaifa “ili Kenya iweze kufikia maendeleo katika sekta zote za uchumi.”
from Taifa Leo https://ift.tt/6kAnTmv
via
IFTTT