Papa Leo XIV amteua Askofu Mkenya kuhudumu Vatican

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Leo XIV amemteua Askofu Mkenya kuwa mwanachama wa asasi moja muhimu ya Vatican inayomsaidia kuongoza Kanisa hilo.

Askofu Kitogho Lagho anayeongoza Dayosisi ya Kanisa Katoliki Malindi sasa atahudumu katika kamati kuhusu mahusiano kati ya madhehebu duniani (Vatican Dicastery for Interreligious Dialogue).

Kufuatia uteuzi huo uliotangazwa Ijumaa, Julai 4, Lagho atapata nafasi ya kipekee ya kuchangia uongozi wa Kanisa Katoliki kutoka makao makuu Vatican.

Kamati ya "The Vatican Dicastery for Interreligious Dialogue" ni mojawapo ya asasi ya usimamizi iliyoko chini ya Asasi Kuu inayojulikana kama, 'Roman Curia' ambayo humsaidia Papa kuongoza Kanisa.

Wakati huu, Askofu Lagho anashikilia uongozi katika safu ya juu ya Kanisa Katoliki Nchini Kenya, akihudumu kama Mwenyekiti wa Tume kuhusu Mazungumzo na Umoja kati ya Madhehebu (CIRDE) katika Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB).

Aidha, yeye ni Mwenyekiti wa Barasa la Madhehebu Nchini Kenya (IRCK), asasi ambayo huendeleza mahusiano mazuri kati ya madhehebu nchini Kenya.

Askofu Lagho, ambaye alizaliwa mnamo Machi 23, 1958, alitawazwa kuwa shemasi (deacon) mjini Mombasa mnamo Desemba 21, 1985.

Baadaye alitawazwa kuwa padre mnamo Aprili 25, 1987, bado akiwa Mombasa.

Baadaye aliteuliwa kuwa Askofu wa Malindi mnamo Desemba 28, 2020 na kutawazwa mwaka uliofuatwa mnamo Machi 19, 2021.

Askofu anatarajiwa kupeleka tajriba yake katika kupalilia mahusiano kati ya madhehebu duniani aliyoipata katika majukumu sawa na hayo nchini Kenya.



from Taifa Leo https://ift.tt/3XA0Dox
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post