Mauaji Saba Saba: Dunia yamulika Kenya

OFISI ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imetoa wito wa uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusu mauaji ya Wakenya 31 wakati wa maandamano ya kuadhimisha Siku ya Saba Saba yaliyofanyika Julai 7. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, katika taarifa aliyotoa jana, alitaja mauaji hayo kama 'yanayotia wasiwasi mkubwa' kwani yametokea chini ya wiki mbili baada ya vifo vya waandamanaji wengine 15 katika maandamano ya Juni 25. Türk alielezea wasiwasi wake kuhusu matumizi ya risasi, risasi za mpira, gesi ya kutoza machozi, na magari ya maji ya mwasho dhidi ya waandamanaji wakidumisha amani jijini Nairobi na maeneo mengine 16. Kwa mujibu wa kamishna huyo, polisi wanapaswa kutumia nguvu pale tu inapokuwa lazima kabisa kulinda maisha dhidi ya tishio la wazi. Akiwalaumu polisi kwa ukatili, Türk pia alieleza hofu yake kuhusu visa vya uporaji na uharibifu wa mali uliofanywa na watu ambao alisema bado hawajatambuliwa na maafisa wa usalama wa Kenya. "Tunasikitishwa sana na mauaji ya angalau watu 10 yaliyotokea jana (Jumatatu), pamoja na uharibifu wa mali nchini Kenya, polisi walipokuwa wakijibu maandamano katika mji mkuu Nairobi na maeneo mengine 16," alisema Türk. "Ni jambo la kusikitisha kwamba matukio haya ya hivi karibuni yanatokea chini ya wiki mbili baada ya waandamanaji 15 kuripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa jijini Nairobi na sehemu nyingine za Kenya Juni 25," aliongeza. Ili kuzuia vifo zaidi, Kamishna Mkuu alitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na kukamatwa kwa wote waliohusika, akiongeza kuwa vitendo hivyo vya mauaji vinakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu. Katika taarifa yake, alieleza kuwa ofisi yake iko tayari kusaidia serikali ya Rais William Ruto katika kuharakisha mchakato wa kushughulikia uhalifu uliotokea wakati wa maandamano ya Siku ya Saba Saba. Taarifa ya Kamishna huyo wa Umoja wa Mataifa inajiri kufuatia maandamano ya Jumatatu ambayo kulingana na polisi yalisababisha vifo vya Wakenya 11 na majeraha mabaya kwa zaidi ya maafisa wa polisi 52. Maandamano hayo, ambayo yalifanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi, yalikuwa ni kuadhimisha miaka 35 ya mapambano ya kupigania demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya, ambayo yalifanyika Julai 7, 1990. Hata hivyo, maandamano hayo ambayo yaliongozwa zaidi na vijana wa Kenya, yalikumbwa na vurugu baada ya polisi kukabiliana na waandamanaji, na kusababisha vifo, uharibifu wa mali, na uporaji. Muda mfupi baada ya maandamano hayo, Huduma ya Polisi ya Kitaifa (NPS), kupitia kwa msemaji wake Muchiri Nyaga, ilitoa taarifa ya kuwasifu maafisa wake kwa kuonyesha ustahimilivu na ustadi.


from Taifa Leo https://ift.tt/QveKiCE
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post