Hivi kumbe hamnijui, afoka Ruto akiahidi kusababishia wazua ghasia ulemavu wa milele

RAIS William Ruto jana alionya upinzani kuwa hataendelea kuvumilia kile alichotaja jaribio la kumngóa mamlakani kupitia msururu wa maandamano, akisema sasa amejiandaa kukabiliana nao peupe kuzuia nchi kusambaratishwa na ghasia.

Kiongozi wa nchi alisema amekuwa kimya kwa kipindi kirefu na kujizuia kukabiliana na wapinzani wake lakini sasa hawezi kuendelea kuvumilia zaidi jaribio la kumwondoa mamlakani kwa njia zisizo za kikatiba.

“Hii ni nchi ya demokrasia na nataka kuwaambia wale ambao wanasema wana uwezo wa kutumia njia zisizo za sheria, ghasia kabla ya 2027 kubadilisha utawala huu kuwa wajaribu,” akasema Rais.

Alizungumza hayo akiwa katika hafla ya kukagua ujenzi wa nyumba za polisi eneo la Kilimani, Nairobi.

Akionekana kujawa na ujasiri wa aina yake, Rais alishangaa kwa nini maasi kama haya sasa yanaendelezwa katika utawala wake ilhali changamoto za nchi zilianza enzi za watangulizi wake.

“Moi alikuwa Rais wa Kenya kama tu Kenyatta, Kibaki na Uhuru. Mbona uadui huu? Mbona hawakufanya hivi kwa Kibaki au Uhuru? Wanalenga nini na ukosefu huu wa heshima? Sisi sote ni Wakenya,” akaongeza.

Kauli ya Rais Ruto sasa inafungua ukurasa mpya wa vita vya kisiasa dhidi ya wapinzani wake ambao wamekuwa wakiunga maandamano dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.

Katika maandamano yaliyofanyika Jumatatu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saba Saba, Wakenya 31 waliripotiwa kuuawa kwa mujibu wa takwimu ambazo zilitolewa na Shirika la Kitaifa la Kutetea Haki za Kibinadamu (KNCHR).

Awali, kwenye maandamano ya Juni 25 ya Gen Z, Wakenya 16 waliaga dunia kwa mujibu wa shirika hilo ingawa serikali ilisema ni Wakenya 10 pekee walifariki.

Kando na mauaji hayo, kumekuwa na uharibifu wa mali na uporaji huku maafisa wa usalama wakilemewa jijini Nairobi na maeneo mengi ukanda wa Mlima Kenya.

Rais alisema maandamano dhidi yake yanayochochewa na upinzani ilhali changamoto kama ukosefu wa vijana hazikuanza wakati wa utawala wake. Alidai upinzani ndio umekuwa ukidhamini kauli ya ‘Ruto Aende’ ilhali amehudumu kwa miaka miwili pekee na hajapewa muda wa kutekeleza miradi aliyoahidi Wakenya wakati wa kampeni.

“Hawa ni watu ambao wanawachochea vijana waharibu mali na kuchoma biashara za watu wakisema wanaandamana kwa sababu ya ukosefu wa kazi. Ukosefu wa kazi ulianza wakati wa Rais Ruto?” akauliza.

Kuchemka kwa rais peupe kulitokea huku Kiongozi wa PLP Martha Karua akihojiwa na kituo kimoja nchini Jumanne usiku, akisema si lazima amalize muhula wake hadi 2027.

“Kuchaguliwa si cheti cha kumiliki ardhi ambacho unatufunikia nyuso, una muhula lakini unaweza kuondolewa. Kumbuka kwamba, mwaka jana ulitimuliwa na maandamano ya Gen Z na utawala wako unaningínia,” akasema Bi Karua.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo anasema rais anahisi amedharauliwa, kudhalilishwa na viongozi wa Mlima Kenya.

Hata hivyo, anapata ujasiri wa kuwakabili kutokana na uungwaji mkono ambao sasa anapata kwenye ngóme za Kinara wa Upinzani Raila Odinga.

“Ukabila una nguzo sana kisiasa nchini na upinzani unatumia kigezo hicho kumpiga vita Rais. Vijana nao wanataka changamoto za nchi zitatuliwe na upinzani unaonekana kutumia hilo kusukuma ajenda zake,” akasema Bw Bigambo.

“Ruto anastahili kukoma kuwasikiza wapinzani na awajibike kwa taifa kwa sababu akiendelea kujibizana nao nayo siasa zitazidi kunoga na miradi ikwame,” akaongeza.

Japo Rais Ruto alionekana kutikiswa na maandamano, alidai baadhi ya vijana wamekuwa wakilipwa na wapinzani wake ili kuharibu mali ya serikali.

“Nimekuwa nikinyamaza na kuwavumilia lakini sasa yametosha. Wale ambao wanavamia vituo vya polisi wameamua vita dhidi ya Kenya na hatutakubali hilo,” akasema.

Alisisitiza kuwa hakuna aliye juu ya sheria na serikali itakamata wanaowalipa vijana kupora huku akiwapa polisi ruhusa wawapige wahalifu hao risasi miguuni.

“Mtu ambaye anaenda kuchoma biashara ya mtu mwingine, mtu ambaye anachukua moto anaenda kuchoma mali ya watu wengine, mtu kama huyo apigwe risasi mguu, aende hospitali na akisha apone aende kortini. Wasimuue, lakini wampige mguu uvunjike,” Ruto said.

Huku Rais akilalamika kuwa kuna nia ya kumpokonya minofu, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua naye alimwaahidi kivumbi kikali mnamo 2027.

“Hakuna anayetaka kupindua serikali yako au kuchukua mamlaka kupitia njia zisizo za kikatiba. Sisi tunataka kukutoa ikulu kupitia kura ya 2027,” akasema Bw Gachagua.

Naibu huyo wa rais wa zamani alisema madai ya Rais ni njama ya kuondoa umakinifu wa Wakenya kwenye dhuluma za polisi wakati wa maandamano.

“Tunataka uhudumu muhula wako mmoja wala hakuna kiongozi anayepanga kukutimua kupitia mapinduzi. Tunataka kupambana na wewe debeni mnamo 2027,” akaongeza.

Bw Gachagua alitetea tawala zilizopita akisema hazikuua au kuteka asasi za kikatiba jinsi Rais Ruto alivyofanya huku akidai kuna njama inayoendelea ya kulemaza eneo la Mlima Kenya kiuchumi kwa kupinga serikali ya Rais Ruto.



from Taifa Leo https://ift.tt/dUD7bvA
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post