Vijana wa Lamu waliopanga kuandamana walivyojikuta wakiimba sifa za Kindiki

UJIO wa Naibu Rais, Prof Kithure Kindiki kisiwani Lamu Jumatatu ulifaulu kufisha azma au ndoto ya baadhi ya vijana ambao awali mipango yao ilikuwa ni kujumuika na wenzao wa maeneo mengine ya Kenya katika maandamano ya Saba Saba.

Siku ya Jumatatu, Julai 7 ilishuhudia maelfu ya vijana kwenye baadhi ya miji ya Kenya walioandamana kuadhimisha miaka 35 ya Saba Saba-yaani Julai 7, 1990.

Hii ni tarehe ambayo Wakenya walijitokeza kudai kurejeshewa mfumo wa vyama vingi vya siasa na demokrasia chini ya utawala wa Rais Mstaafu, hayati Daniel Toroitich arap Moi.

Wito wa kujitokeza kwa maandamano ya Saba Saba ya Jumatatu hata hivyo ilikuwa ni kukashifu maovu serikalini pamoja na ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji, hasa mauaji ya vijana wa Gen Z ambayo tayari yametekelezwa nchini kufikia sasa.

Kufikia Jumatatu jioni, polisi walitoa taarifa kwamba watu kumi walikuwa wameuawa ilhali maafisa 52 wa polisi na raia 11 wakijeruhiwa kwenye maandamano hayo.

Watu wapatao 567 walikamatwa kwenye maandamano hayo ya Saba Saba.

Huku ghasia, mauaji, maajeruhi na kamatakamata ya polisi dhidi ya waandamanaji ikiendelea maeneo mengi ya Kenya, kisiwani Lamu mambo yalikuwa tofauti.

Hapa, shamrashamra za kumlaki Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki na timu yake zilishamiri kila upande, hivyo kuteka nyoyo na fikra za vijana wa Lamu.

Baadhi ya waliohojiwa na Taifa Leo walionekana kuzama kwenye bahari ya furaha, wengine wakidai hata hiyo Saba Saba hawaifahamu ila Prof Kindiki pekee.

[caption id="attachment_174732" align="alignnone" width="2560"] Kiongozi wa wengi kwenye Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung'wah, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Lamu, Bi Muthoni Marubu, Naibu Rais Kithure Kindiki, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir wakati walipokuwa wakiondoka kisiwani Lamu Jumatatu baada ya kuhutubia umma eneo la Mkunguni Jumatatu, Julai 7,2025. Picha|Kalume Kazungu[/caption]

Badala ya kubeba mabango ya jumbe zinazofungamana na maandamano ya Saba Saba, vijana hao hao walijipata kutekwa wazimawazima, hivyo kuishia kuanika mabango ya kumkaribisha Prof Kindiki.

Miongoni mwa jumbe zilizokuwemo kwenye mabango hayo ni pamoja na ‘Iko Love Kisiwani,’ ‘Karibu Amu Kindiki Mfalme Wetu,’ ‘Twakupenda Kindiki,’ ‘Ruto, Kindiki Kumi Bila Breki’ nakadhalika.

“Kwanza hatujui hiyo Saba Saba ni nini hapa Lamu. Lamu ni amani tupu. Twasema Kindiki karibu. Wewe ndiwe tunakuangalia,” akasema Bw Omar Bashali.

Athman Swaleh alisema licha ya wao kujumuika na wenzao wa maeneo mengine ya Kenya kushiriki maandamano ya kuwakumbuka Gen Z waliouawa nchini Juni 25, safari hii hawangeandamana Jumatatu kuadhimisha Saba Saba na wenzao kama njia mojawapo ya kuwaenzi viongozi waliotembelea kisiwa cha Lamu.

“Watu wa Lamu ni wenye ukarimu na heshima. Hata tukashiriki maandamano, hapa kwetu huwa ni amani tupu. Hatutaki fujo. Na ndiyo sababu leo tumeamua kutii ziara ya Naibu Rais, Prof Kindiki na wenzake waliofika hapa kwa kutoshiriki Saba Saba ila hilo halimaanishi kwamba tuko kinyume na wenzetu wengine nchini,” akasema Bw Swaleh.

Kiongozi wa vijana na mwanaharakati wa kijamii Lamu, Bw Yunus Issakia pia alionekana kuzama ndani ya shamrashamra na midundo ya kumkaribisha Prof Kindiki.

Katika ujumbe wake, Bw Issakia aliwashauri vijana kuzingatia amani na kuepuka kuendeleza vurumai, uharibifu wa mali na miundomsingi nchini.

“Tumeamua hatutatumiwa. Kenya ni nchi yetu sote na tukiiharibu hatuna kwingine pa kwenda. Vijana wenzangu tusiharibu au kuchoma nchi yetu. Lazima tufanye kila jambo kwa utaratibu na amani,” akasema Bw Issakia.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kwamba mbali na kisiwa cha Lamu, miji mingine mikuu ya eneo hilo, ikiwemo Mpeketoni, Witu, Hindi, Mokowe, Shella, Faza, Kizingitini, Ndau, Mkokoni, Kiwayu, Kiunga na kwingineko, kote kulishuhudia utulivu na Amani.

Akihutubia umma eneo la Mkunguni kisiwani Lamu, Prof Kindiki alichukua fursa hiyo kuwarai Wakenya, ikiwemo viongozi, vijana na wengineo kudumisha amani.

Pia aliwataka kutafuta njia mbadala na za amani, ikiwemo majadiliano ili kutatua shida za kitaifa badala ya ghasia, maandamano na Saba Saba.

“Ninawarai Wakenya wenzangu na viongozi. Tutafute mbinu mbadala na ya amani kutatua shida za kitaifa badala ya vurugu, uchochezi, maandamano na Sabasaba. Haitawezekana kujenga nchi ya Kenya kupitia vita na vurumai za kila mara na kuhatarisha amani, umoja na usalama wa kitaifa,” akasema Prof Kindiki.

Alisema ni haki ya kikatiba kwa wananchi kuwa na maoni tofauti kuuhusu uongozi au serikali.

“Wale wenye maoni tofauti kuhusu serikali, mko na haki kufanya hivyo kikatiba ila lazima yote yatendeke kwa njia ya amani. Najua mnakubaliana na mimi wenzangu kwamba hakuna kitu cha thamani katika taifa au ulimwengu kuliko usalama na amani,” akasema Prof Kindiki.



from Taifa Leo https://ift.tt/IpGxivc
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post