JAPO viongozi wakuu serikalini wamekuwa wakiamrisha polisi wawaue waandamanaji, itawalazimu maafisa wa usalama wafuate amri hiyo kwa tahadhari baada ya afisa aliyedaiwa kumuua mwandamanaji kuonekana jana akibubujikwa na machozi, akipambana kivyake na mashtaka ya mauaji kortini.
Afisa wa polisi aliyenaswa kwenye kamera akimpiga risasi muuzaji wa barakoa Boniface Kariuki Mwangi, jana alilia machozi na kuandamwa na masikitiko akiwa pweke kizimbani.
Polisi huyo wa cheo cha konstebo Klinzy Barasa alifikishwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Margaret Muigai baada ya Bw Kariuki kuaga Juni 30 katika Hospitali Kuu ya Kenyatta.
Marehemu ambaye mauti yake yalizua ghadhabu ya umma anatarajiwa kuzikwa leo katika Kaunti ya Murangá.
Afisa mwingine Duncan Kiprono ambaye alikuwa na Barasa wakati wa tukio hilo aliachiliwa huru.
Marehemu Kariuki aliuawa wakati wa maandamano ya Gen Z mnamo Juni 25, 2024 ambapo vijana hao walikuwa wakiadhimisha mwaka mmoja tangu kuuawa kwa wenzao 60.
[caption id="attachment_174782" align="alignnone" width="2000"]
Bw Kiprono naye aliachiliwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuambia korti hakukuwa na ushahidi wowote wa kuunga mashtaka ya mauaji dhidi yake.
Aliondoka kortini akiwa ameandamana na mawakili wake na jamaa zake wachache huku akimwaacha mwenzake akipambana na mkondo wa sheria.
Barasa alifikishwa mbele ya Jaji Muigai ambaye alimfahamisha kuhusu mashtaka ya mauaji dhidi yake.
“Hii ndiyo mara ya kwanza Barasa anafika kortini na hahitajiki kukubali au kukanusha mashtaka. Mahakama inamfahamisha tu kuhusu mashtaka dhidi yake,” kiongozi wa mashtaka akaambia jaji.
Kiongozi huyo wa mashtaka pia aliomba korti isiruhusu Barasa kukanusha au kikiri mashtaka dhidi yake hadi afanyiwe uchunguzi wa akili kabla ya kushtakiwa.
Jaji Muigai aliambia afisa huyo wa polisi kuwa, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) aliwasilisha mashtaka ya mauaji dhidi yake.
Hii ni baada ya kumuua marehemu Kariuki kwenye barabara ya Moi Avenue, Nairobi mnamo Juni 25, 2025.
Afisa huyo sasa atarudi mahakamani baada ya siku 14 na jaji aliamrisha asukumwe katika gereza la Industrial Area Prisons, Nairobi kisha apimwe akili kwenye Hospitali ya Mathare kabla ya siku ya kurejeshwa kortini.
Barasa akipambana mahakamani na kubeba msalaba wake kivyake, viongozi serikalini nao wamekuwa wakiwaagiza polisi wawaue waandamanaji ambao wanashiriki uporaji au kuvamia kituo cha polisi au afisi za serikali.
Rais William Ruto, Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Bungeni Nelson Koech ni kati ya viongozi ambao wamekuwa wakiwahimiza maafisa wa polisi kuua waandamanaji.
Mnamo Alhamisi, Rais Ruto alidai wahuni wa kushiriki uporaji wamekuwa wakilipwa na wapinzani wake na akataka polisi wawapige risasi miguuni ili wapambane na kesi mahakamani wakiwa na maumivu.
“Mtu ambaye anaenda kuchoma biashara ya mtu mwingine, mtu ambaye anachukua moto anaenda kuchoma mali ya watu wengine, mtu kama huyo apigwe risasi mguu, aende hospitali na akisha apone aende kortini. Wasimuue, lakini wampige mguu uvunjike,” akasema Rais Ruto akiwa jijini Nairobi.
Bw Murkomen naye mnamo Juni 28 alitoa amri kuwa polisi wanastahili kuwaua waandamanaji wanaovamia kituo cha polisi lakini akakanusha matamshi hayo baadaye.
"Na tumeambia polisi mtu yeyote atayekaribia kituo cha polisi piga yeye risasi," akasema Murkomen akikagua uharibifu na uporaji ambao ulikuwa umetokea jijini Nairobi baada ya maandamano ya Gen Z.
Hata hivyo, alikanusha baadaye kuwa aliwaambia polisi wachukue amri kutoka kwa mtu yeyote.
“Sikusema mtu yeyote anastahili kupigwa risasi. Sikuandika sheria lakini inasema kuwa polisi akikabiliwa na hatari, lazima atumie bunduki yake,” akasema Bw Murkomen.
Bw Koech ambaye ni mbunge wa Belgut naye Alhamisi video yake ilisambaa mitandaoni akiunga kauli ya Rais Ruto kuwa wahuni wapigwe risasi.
“Nataka nimshukuru Rais Ruto kwa kutoa amri ya kupiga risasi lakini bila kuua. Mimi nasema piga risasi na uue kwa sababu haiwezekani mtu anakuja kwenye biashara yako akiwa amejihami na utaniambia hutampiga risasi na kumuua,” akasema Bw Koech.
Mbunge huyo alisema kuwa katiba na sheria zinazoongoza idara ya polisi zinawapa mamlaka ya kutumia bunduki zao panapotokea hatari.
from Taifa Leo https://ift.tt/ezx0OfC
via IFTTT