Jinsi hatua ya kijana kujipiga selfie na maafisa ilivyoishia katika kupigwa risasi Nyamira

MNAMO Jumanne Julai 9, Brian Arisa, 19, aliondoka nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji cha Kenyoro, eneo bunge la Mugirango Kaskazini, Kaunti ya Nyamira mwendo wa saa nne asubuhi hivi. Kama ilivyo kawaida yake, alifululiza hadi kituo cha kibiashara cha Itibo, ambacho kiko mita chache kutoka nyumbani kwao kukutana na marafiki zake. Lakini kabla hajafika katika kituo hicho cha maduka, alisikia vurumai za kundi la watu waliokuwa wakizua ghasia ambao walikuwa wakielekea upande sawia na wake. [caption id="attachment_174793" align="alignnone" width="1280"] Brian Arisa,19, (aliyevalia tishati nyekundu) katika picha hii ya selfie aliyopiga na maafisa wa polisi waliokuwa wakituliza maandamano ya wanafunzi wa chuo anuwai cha kitaifa cha Nyamira mnamo Jumanne wiki hii. Arisa anasemekana kupigwa risasi na mmoja wa maafisa hao ambaye hakufurahia kitendo cha yeye kuwapiga picha. Familia ya kijana huyo sasa inalilia haki ya mwanao aliyeaga dunia kutokana na majeraha ya risasi hiyo. Picha|Hisani[/caption] Alipouliza kilichokuwa kikifanyika, Arisa aligundua kuwa kundi hilo lilikuwa la wanafunzi wa chuo kikuu anuwai cha Nyamira. Kulingana na Bi Mary Otwori, mkazi wa eneo hilo, wanafunzi hao walikuwa wakiandamana kuelekea afisi ya Mwakilishi wa Wadi ya Itibo (MCA), wakitaka kupewa maelezo kuhusu hali mbaya ya barabara nyingi katika eneo hilo hasa zile zinazopita karibu na chuo hicho. "Wanafunzi hao walimshutumu MCA huyo kwa kile walidai ni kufanya machache katika kuboresha barabara za eneo hili, na zaidi hasa zile zilizo karibu na taasisi yao. Walidai kuwa kwa kuwa chuo chao kiliinuliwa hadhi hivi majuzi na kuwa cha kitaifa, kilifaa kuwa na barabara bora zinazoingia na kutoka humo, ikiwa ni pamoja na zile zinazoelekea katika vyumba vyao vya malazi," Bi Otwori alisema. Aliongeza, "walilalamika kuwa MCA wa eneo hilo amepuuza barabara nyingi zinazoingia kwenye taasisi yao na kwa hivyo, walikuwa wakitatizika hasa wakati huu wa mvua nyingi," Walipokuwa wanaendelea na maandamano yao, wanafunzi hao walitekeleza uharibifu uliohusisha uporaji wa mali na vitu vingine vingine walivyokutana navyo njiani. Wakazi wa eneo hilo walipoona kwamba watapata hasara kutokana na maandamano ya wanafunzi hao, waliwaarifu maafisa wa polisi ambao waliwasili na kuanza kuwakabili. [caption id="attachment_174794" align="alignnone" width="1200"] Wafanyabiashara katika soko la Itibo wakagua hasara waliyoipata baada ya wanafunzi wa chuo anuwai cha kitaifa cha Nyamira kuteketeza vibanda vyao. Picha|Wycliffe Nyaberi[/caption] Nao wanafunzi walipoona maafisa hao, walichemka na hapo mapambano kati ya pande hizo mbili yalianza. Maafisa wa polisi waliwarushia wanafunzi hao vitoa machozi kuwatawanya. Kwa muda huo wote wa makabiliano, Arisa alikuwa amesimama kwa mbali, akitazama kwa makini na kurekodi matukio ya siku hiyo kwenye simu yake. Baadaye alisogea karibu na walipokuwa maafisa hao na kuanza kuchukua picha za selfie na maafisa hao. Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, inasemekana hatua hiyo ya Arisa kupiga picha zao haikumpendeza mmoja wa maafisa waliokuwa wakiwatuliza wanafunzi hao na inasemekana ugomvi ulizuka baina yao. Kwa kuhofia kwamba maafisa hao wangemkamata, kijana huyo aliondoka pale walipokuwa maafisa hao na kutaka kurudi nyumbani. Kulingana na Bw Dominic Mokaya, Arisa hakuenda mbali sana kwani afisa mmoja alimfyatulia risasi. "Alikuwa akiwarekodi maafisa waliokuwa wakiwakabili wanafunzi. Maafisa hao hawakufurahia picha alizowapiga Arisa na walimwamuru aondoke kwao. Lakini kabla hajaenda umbali sana, afisa mmoja anayejulikana kama Robah,  alimpiga risasi tumboni na kumwangusha chini," Bw Mokaya alidai. Walipoona kwamba Arisa amepigwa risasi, wanafunzi hao walipandwa na mori zaidi na kuelekea katika kituo cha kushika doria cha Itibo na kukiteketeza. Stakabadhi na vitu vingine muhimu vya polisi viliharibiwa katika mchakato huo. Wanafunzi hao pia walichoma vibanda vya wafanyabiashara vilivyokuwa karibu na kituo hicho huku wakimsaka afisa aliyempiga Arisa risasi. [caption id="attachment_174795" align="alignnone" width="1080"] Wazazi wa Brian Arisa Milcah Gesare na James Moriasi katika kijiji cha Kenyoro, Nyamira. Picha|Wycliffe Nyaberi[/caption] Kuona kwamba wanazidiwa, maafisa hao walitoroka eneo hilo. Hali ya taharuki ilikuwa ingali bado imetanda katika soko hilo la Itibo siku moja baada ya kijana huyo kupigwa risasi. Mita chache kutoka soko hilo ni kijiji cha Kenyoro ambako Arisa alitoka. Hali ya huzuni ilitanda huku wazazi na jamaa wa Arisa wakijitahidi kukubaliana na kilichowasibu. Wazazi wa marehemu, Bw James Moriasi na Milcah Gesare walilia kwikwikwi walipokuwa wakisimulia jinsi mtoto wao alivyouawa. Wazazi hao waliozeeka waliomba Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuingilia kati katika suala hilo na kuhakikisha kwamba familia yao inapata haki. [caption id="attachment_174796" align="alignnone" width="1280"] Kituo cha polisi cha Itibo, kilichoteketezwa moto na wanafunzi wa chuo anuwai cha kitaifa cha Nyamira baada ya maandamano yao. Picha|Wycliffe Nyaberi[/caption] "Kwa nini walimuua mwanangu kwa kupiga picha tu? Kumuua ilikuwa sawa na kunimaliza kwa sababu licha ya umri wake mdogo, alikuwa akinitunza mimi na mamake. Ni nani sasa atatusaidia katika uzee wetu? IPOA iko wapi? Tunataka wachukue suala hili na kubaini kilichotokea," Bw Moriasi alisema. Binamu wa Arisa, Christine Aroni, ambaye ni wakili, alitoa wito kwa serikali kutokana na ongezeko la visa vya mauaji ya kikatili ambayo yametawala nchini hivi karibuni. Bi Aroni alisema sheria hairuhusu polisi kuwapiga risasi na kuwaua raia wasio na silaha. "Alichokuwa nacho ni simu yake tu. Kwa nini walimpiga risasi? Kesi za mauaji ya kiholela zinaongezeka humu nchini na hili lazima lifikie kikomo," Bi Aroni aliongeza. Baada ya kupigwa risasi tumboni, Arisa alikimbizwa katika hospitali ya karibu lakini baadaye, alifariki dunia.

from Taifa Leo https://ift.tt/Aae2bNz
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post