Tukio la mtawa akimzaba kofi mwenzake wakibishana hadharani laudhi waumini

WAUMINI wa Kanisa Katoliki na umma kwa jumla wameeleza hasira zao kutokana na kisa ambapo mtawa mmoja wa Kanisa Katoliki alimpiga kofi mwenzake baada ya mabishano kuzuka kati yao.

Kisa hicho kilinaswa kwenye video iliyosambaa mitandaoni, iliyorekodiwa kwa simu ya mkononi. Mtu aliyenasa video hiyo ndiye mwathiriwa wa shambulio hilo.

Katika video hiyo, mtawa aliyevalia mavazi rasmi na rozari shingoni, anaonekana akimkabili mwanamke aliyesimama mlangoni mwa chumba kimoja ndani ya jumba la watawa.

Muumini mmoja wa Kanisa Katoliki katika Kaunti ya Homa Bay aliambia Taifa Leo kuwa tukio hilo lilifanyika katika makao ya watawa.

Katika video hiyo, mtawa mkubwa kwa cheo anasikika akimhoji mwenzake kuhusu kosa alilofanya.

“Unaona haujafanya kitu. Unajua wewe ni mdogo lakini vitu unanifanyia hapa unaona kama ni nini?” alisikika akisema kabla ya kumpiga kofi kwenye shavu.

Wakati wa shambulio hilo, mwathiriwa aliyekuwa akirekodi video hiyo alisikika akiuliza kwa mshangao kwa nini anapigwa mbele ya wafanyakazi waliokuwa eneo hilo.

“Nimekufanyia nini? Kwa nini unanipiga mbele ya wafanyakazi?” aliuliza huku mtawa mkubwa akitishia kumpiga zaidi.

Katika mzozo huo, alimtaka yule mdogo amkabidhi mafuta.

“Usikuje chini kama haujapeana hiyo mafuta,” alisikika akisema kwa sauti ya ukali, huku akiendelea kutoa vitisho zaidi.

Aliendelea kusema: “Unajua huyu mtoto ni mjinga sana. Piga simu Asumbi,” akimaanisha kituo cha kidini cha Kanisa Katoliki cha Asumbi.

Watu kadhaa wanaonekana wamesimama karibu na tukio hilo, wakitazama mzozo huo bila kuingilia kati.

Katika taarifa rasmi, Shirika la Watawa la Franciscan Sisters of St Joseph limesema tukio hilo ni la kusikitisha.

Kiongozi Mkuu wa Shirika hilo, Sr Mary Goretty Ochieng, alisema anafahamu kuhusu tukio hilo ambapo mmoja wa watawa wao alimpiga mwingine mdogo.

“Kitendo hicho ni kosa la mtu binafsi na hakiwakilishi maadili ya watawa wa Franciscan Sisters of St Joseph. Tunasikitika sana kwa madhara yaliyompata mtawa huyo, pamoja na fedheha ambayo tukio hilo limesababisha kwa shirika letu, Kanisa na jamii kwa jumla,” alisema Sr Ochieng kwenye taarifa hiyo.



from Taifa Leo https://ift.tt/B0pKIAF
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post