Wanasayansi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Afya Kenya (Kemri) kwa ushirikiano na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo ya Israel, wanasaka njia bunifu za kupambana na uvamizi wa konokono katika mashamba ya mpunga ya Mwea, Kirinyaga.
Konokono hao wamekuwa ni tishio kubwa kwa wakulima wa mpunga na afya ya umma.
Roseline Njeri, mkulima wa mpunga mwenye uzoefu wa miaka 23, anasema konokono hao walianza kuharibu mazao yake tangu mwaka 2020.
“Tulianza kuona konokono hawa mwaka 2020, na wamekuwa janga. Mara unapoanzia kupanda, wao tayari wako tayari kula,” anasema Roseline.
Konokono hawa wanaharibu mimea ya mpunga, na huenea kwa kasi kiasi cha kupunguza uzalishaji wa wakulima, huku dawa za kuwadhibiti zikishindwa na kuathiri mazingira.
Dk Geoffrey Maina kutoka Kemri anafafanua kuwa konokono hao wanasababisha mambukizi wa ugonjwa hatari wa ubongo unaojulikana kama eosinophilic meningitis, unaosababishwa na kirusi kutoka kwa konokono hadi kwa binadamu.
Kupitia mradi wa majaribio wa kutumia viumbe hai, wanasayansi wanatumia kamba wa maji safi wanaokula konokono hawa kwa wingi, kuondoa hatari ya uvamizi huo na kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa kichocho unaosababishwa na konokono wa aina nyingine.
Profesa Amir Sagi wa Chuo Kikuu cha Ben Gurion, kiongozi wa mradi, anasema ni mara ya kwanza duniani kutumia mbinu hii katika shamba la mpunga.
“Tunatumia kamba hawa kwa sababu ni wadudu hodari wanaokula konokono wengi haraka na kwa kiasi kikubwa. Pia watasaidia kupunguza maambukizi ya bilharzia,” anasema Profesa Sagi.
Wanasayansi wana mpango wa kuanzisha kiwanda kidogo cha kukuza kamba nchini Kenya, na wanatafuta ushirikiano wa wakulima wanaofuga samaki ili mradi huu uweze kufanikishwa.
Dk Ibrahim Mwangi wa Kemri anasema kuwa mbinu hii itaongeza ufanisi wa dawa zilizopo na kusaidia kudhibiti ugonjwa wa kichocho kwa njia ya asili na endelevu.
Wakulima kama Roseline wanatarajia kuwa suluhisho hili la kisayansi litaleta mabadiliko makubwa katika kilimo cha mpunga na afya ya jamii ya Mwea.
from Taifa Leo https://ift.tt/lbmB7JE
via IFTTT