Wizara ya Elimu imefichua zaidi ya wanafunzi 50,000 hewa katika shule za upili kote nchini, ikifichua udanganyifu mkubwa katika rekodi za usajili na kuibua maswali kuhusu uadilifu wa mgao wa fedha za serikali kwa taasisi hizo.
Idadi hii inamaanisha hasara ya zaidi ya Sh1.1 bilioni kila mwaka, na jumla ya Sh4.4 bilioni ambazo huenda zilitumiwa vibaya katika kipindi cha miaka minne.Katibu wa Elimu ya Msingi, Prof Julius Bitok, aliambia Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa kuwa idadi hiyo imepatikana hata kabla ya ukaguzi wa kitaifa kukamilika, ukaguzi ambao unalenga shule zote za sekondari nchini.
“Hadi sasa, tumefanikisha usambazaji wa fedha kwa shule takriban 17,500—shule 5,732 za sekondari, 5,525 za sekondari msingi na 600 za mahitaji maalum. Tumegundua kuwa zaidi ya wanafunzi 50,000 wa sekondari hawawezi kuthibitishwa. Idadi hazilingani.
Shule za msingi na sekondari msingi zinaonekana kuwa na wanafunzi zaidi wasioweza kuthibitishwa,” alisema Prof Bitok.
Alisema kuwa kwa muhula wa tatu wa mwaka wa fedha 2025/26, serikali imeachilia kiasi kikubwa cha fedha ikiwa ni Sh1.75 bilioni kwa shule za msingi (Sh456.4 milioni zikiwa tayari zimepelekwa shuleni kufikia Septemba 16, 2025), Sh5.7 bilioni kwa shule za sekondari msingi (Sh1.02 bilioni zikiwa zimesambazwa), Sh10.38 bilioni kwa shule za sekondari (Sh5.14 bilioni zikiwa tayari zimetumwa shuleni),Sh40 milioni kwa shule za mahitaji maalum (Sh1.02 milioni zikiwa zimesambazwa).
Fedha za mitihani Sh5.9 bilioni, na jumla ya fedha zilizotolewa hadi sasa ni Sh13 bilioni kati ya Sh23 bilioni zilizotengwa kwa muhula huu.
Prof Bitok alisema kuwa baada ya ukaguzi kukamilika, idadi ya wanafunzi walioko shuleni huenda ikapungua kwa asilimia 10, na vilevile idadi ya shule zinazopokea fedha za serikali.Aliweka wazi kuwa zoezi la kusafisha takwimu ambalo linahusisha shule 32,000 limekamilika kwa asilimia 60.
Takwimu hizo zinatokana na habari aa mfumo wa NEMIS, wakuu wa shule, na wakurugenzi wa elimu katika kaunti ndogo.“Tunalinganisha taarifa kutoka NEMIS, wakuu wa shule, na wakurugenzi wa elimu ili kuthibitisha wanafunzi na shule halali,” alisema Prof Bitok.
from Taifa Leo https://ift.tt/KjPoTya
via IFTTT