Ajabu Rais Kiir akimteua mfu kuongoza jopo la kusimamia uchaguzi wa Desemba

RAIS wa Sudan Kusini Salva Kiir, amekejeliwa kwa kumteua mtu aliyefariki kusimamia jopo la mazungumzo kuhusu uchaguzi utakaofanyika mwezi Desemba.

Hatua hiyo imemfanya rais huyo kuwafuta kazi wafanyikazi wake wawili.

Uteuzi wa Steward Soroba Budia ulitangazwa mnamo Januari 30 ila vyombo vya habari vya taifa hilo vilitangaza kuwa Budia, ambaye alikuwa mwanachama wa chama cha upinzani cha United Democratic Party (UDP), alifariki miaka mitano iliyopita.

Raia wa Sudan Kusini walikejeli uteuzi huo kwenye mitandao ya kijamii.

Bila kutoa maelezo, taarifa kutoka kwa rais huyo kwa vyombo vya habari ilisema kuwa amewafuta kazi katibu wake wa mawasiliano David Amour Major na msimamizi wa ofisi ya rais Valentino Dhel Maluet.

Februari 01, 2026, Amour alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa ofisi ya rais ilitegemea “usahihi na uhakiki kikamilifu wa majina” yaliyowasilishwa na “washikadau” kwa ajili ya kujumuishwa katika jopo hilo.

“Sasa imebainika kuwa uhakiki wa kina haukufanywa na mmoja wa washikadau, jambo lililosababisha makosa haya kutokea kimakosa,” alisema Amour.

Amour hakusema ni nani, na chama cha UDP pia hakijatoa tamko lolote kuhusu suala hilo.

Haijulikani ikiwa taarifa hiyo ilisababisha kufutwa kazi kwa Amour ila kulikuwa na uvumi hapo awali kwamba angefutwa kazi.



from Taifa Leo https://ift.tt/DaSRzjI
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post