Hofu yagubika ODM kwamba itapata makombo kwa UDA kutokana na uhasama

UHASAMA wa ndani kwa ndani ODM unatishia kudhoofisha chama hicho kikubwa kwenye mazungumzo ambayo yamepangwa kati yao na UDA.

ODM ilikuwa ikilenga kutumia umaarufu na uthabiti wake wa kisiasa maeneo mbalimbali pamoja na idadi yake bungeni kudai minofu katika mazungumzo yanayonukia na UDA.

Hata hivyo, Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga na Katibu Mkuu wanayezozana Edwin Sifuna sasa wanaelekea njia tofauti, kila mmoja akiwavutia wafuasi upande wake.

Rais Ruto aliongozwa na nia ya kufanya kazi na ODM kutokana na umaarufu wa chama hicho maeneo ya Nyanza, Pwani, Magharibi, jamii ya Wamasaai na baadhi ya maeneo ya Kaskazini Mashariki.

Hata hivyo, vita vikali kati ya mirengo inayoongozwa na Dkt Oginga na Seneta Sifuna sasa inatishia ushawishi wa ODM na Rais Ruto kunufaika na kura za ngome zake.

Itamlazimu Rais kuwasaka washirika wengine iwapo Bw Sifuna atafanikiwa ‘kuhepa’ na ngome za ODM.

Dkt Oginga kwa upande wake amesema wanalenga kupata wadhifa wa mgombeaji mwenza wa Rais katika mazungumzo yanayoendelea.

Wikendi iliyopita, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki alisema haendi popote huku washirika wake wakisema atasalia naibu rais hadi 2037.

“Naelewa ODM inataka kiti hiki na hilo limesababisha tumbo joto hapa Meru. Hata hivyo, mimi ndiye naibu rais na siendi popote kwa sababu katika siasa mimi si wa kusukumwa tu wala siwezi kutishwa,” akasema Profesa Kindiki akisema matakwa ya ODM ni ‘hewa tupu’.

Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi ambaye yupo kambi ya Bw Sifuna naye anasema ODM inatosha kuwa na mwaniaji wa urais mnamo 2027 badala ya kuinamia Rais Ruto na kusaka mgombeaji mwenza.

“Hatuwezi kuingia kwenye makubaliano ya kisiasa kama chama dhaifu. Wenzetu ndani ya Serikali Jumuishi wanasaka nafasi ambazo hazionyeshi hadhi ya ODM,” akasema Bw Osotsi.



from Taifa Leo https://ift.tt/vDQAxH3
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post