
ALIYEKUWA Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i jana aliahidi jamii ya Abagusii kuwa hatawavunja moyo katika azma yake ya kuwania urais mnamo 2027 huku akijisawiri kama mgombeaji bora zaidi kati ya vinara wenzake ndani ya upinzani. Dkt Matiang’i aliye pia naibu kiongozi wa chama cha Jubilee jana alitawazwa kama mzee wa Abagusii, akiahidi kuwa chini ya uongozi wake, jamii hiyo itavuna matunda ya maendeleo na kuhisi uwepo wao ndani ya serikali. “Ninashukuru sana jamii ya Gusii kutokana na heshima hii niliyopewa. Nawaahidi watu wangu kuwa sitawaangusha,” akasema katika eneo la Ekerenyo. Kutawazwa kama mzee sasa kunamweka Dkt Matiang’i kama msemaji wa kisiasa wa jamii hiyo. Pia hatua hiyo sasa imempa ‘baraka’ ya kuenda nje ya eneo la Gusii kusaka uungwaji mkono kutoka kwa jamii nyingine na kuimarisha nafasi yake ya kutwaa uongozi wa nchi. Baada ya kutawazwa, Dkt Matiang’i alitangaza hadharani kuwa atashirikiana na wenzake katika upinzani mia fil mia. “Nimeamrishwa na wazee wa Abagusii kufanya kazi pamoja na viongozi wengine wa upinzani. Nawaahidi kuhakikisha kuwa kuna umoja wa upinzani,” akasema. Dkt Matiang’i ni mwandani wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee. Ingawa hivyo, katika kambi ya upinzani kumekuwa na uhusiano vuguvugu kati ya Dkt Matiang’i na Bw Kenyatta kwa upande mmoja na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua hasa katika kung’ang’ania udhibiti wa kura za Mlima Kenya. Bw Gachagua amekuwa akisema chama chake cha DCP ‘ndicho kusema’ Mlimani na kutaja Jubilee kama mojawapo ya vyama vya ‘Wilbaro’, kauli inayofasiriwa kuwa inafadhiliwa na mrengo wa Serikali. Mwezi uliopita, Dkt Matiang’i alichemsha kambi ya upinzani kwa kudai kuwa atakubali tu mfumo wa kisayansi wa kuteua mwaniaji wa urais wa upinzani wala si njia nyingine. Jana, Bw Gachagua alimpongeza Dkt Matiang’i na kusema kuwa hatarajea nyumbani mikono mitupu baada ya kuamua kushirikiana na upinzani. “Mtoto wenu huyu ni mwenye bidii na sasa yeye ni kiongozi wa jamii ambayo pia ina bidii. Hatarejea nyumbani mikono mitupu, atarejea akiwa na hadhi,” akasema Bw Gachagua. “Kama jamii, lazima mhakikishe kwamba Dkt Matiang’i anaheshimiwa hapa nyumbani. Hiyo itanisaidia kumvumisha Mlima Kenya,” akaongeza. Alisema jamii ya Abagusii haifai kuendelea kumuunga Rais William Ruto kwa sababu uongozi wake haujawanufaisha kivyovyote. Jana, Bw Gachagua, Dkt Matiang’i, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa na Kinara wa PNU, Peter Munya, waliendeleza misururu ya ziara ambayo ilianza Kusini mwa Bonde la Ufa hadi uwanja wa Gusii. Bw Gachagua aliwaambia wakazi wa kusini mwa Bonde, ngome ya Rais kuwa hawana tatizo na jamii ya Wakalenjin ila wanataka kumwondoa mwanao madarakani kutokana na utendakazi duni. Viongozi hao waliwataka wakazi wa eneo hilo wapigie kura upinzani ili hata serikali ikishindwa 2027 bado watakuwa sehemu ya uongozi utakaokuwa madarakani. Bw Musyoka naye alimtaka Rais Ruto kuimarisha miundomsingi katika eneo lake kabla ya kuwalaumu viongozi kutoka maeneo mengine. “Inashangaza kuwa hakuna mradi wowote wa maendeleo ambao umeanzishwa hapa Kusini mwa Bonde la Ufa huku maeneo mengine yakinufaika,” akasema Bw Musyoka. Bw Wamalwa naye alisikitika kuwa sekta ya afya inaendelea kuporomoka chini ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA) akiahidi kuwa upinzani utanyoosha sekta hiyo ukichukua mamlaka mnamo 2027. Wanasiasa hao pia walihutubia umma katika vituo vya kibiashara mjini Bomet, Mulot, Chebole, Kaplong, Sotik, Ikonge, Keroka, Birongo, Keumbu na Kisii. Juhudi za baadhi ya wahuni kutibua mkutano wao mjini Kisii ziliangukia pua baada ya kukabiliwa na wananchi huku baadhi yao wakiumizwa.
from Taifa Leo https://ift.tt/BOf1IpA
via
IFTTT